USULUHISHI WA MIGOGORO KURAHISISHA UKAMILISHAJI WA MIRADI YA UJENZI KWA WAKATI
Utatuzi wa migogoro kwa kuzingatia sheria, kanuni na masharti ya mikataba ya ujenzi unaweza kupunguza ucheleweshaji wa miradi, kudhibiti gharama na kulinda maslahi ya pande zinazohusika katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi.
Katika kuimarisha uwezo wa wadau katika eneo hilo, Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limeendesha mafunzo ya uendeshaji na Utaratibu wa Usuluhishi wa Migogoro (Conduct and Practice of Arbitration), ambayo yamefanyika Jijini Dar es Salaam, kuanzia Novemba 23 hadi 27, 2026.
Akizungumza wakati wa uendeshaji wa mafunzo hayo mkufunzi, Qs.Elias Kissamo ameeleza kuwa Katika tasnia ya ujenzi, migogoro inayotokana na tafsiri ya masharti ya mikataba, ucheleweshaji wa malipo, mabadiliko ya gharama na muda wa utekelezaji wa miradi inaweza kuathiri ufanisi wa miradi endapo haitapatiwa ufumbuzi kwa wakati hivyo ni muhimu kujua jinsi ya uendeshaji na utaratibu wa usuluhishi wa migogoro, amesema
Aidha mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bi.Rose Mtesigwa Wakili kutoka kampuni ya Bakhresa Food Products Ltd ameongeza kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa sababu yanaongeza maarifa na weledi kwa washiriki katika maswala yote ya usuluhishi wa migogoro.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo washiriki kuhusu misingi ya usuluhishi wa migogoro, taratibu za uendeshaji wa mashauri, uchambuzi wa ushahidi pamoja na utoaji wa maamuzi kwa kuzingatia sheria, haki na weledi.
Kupitia mafunzo hayo, NCC inaendeleza dhamira yake ya kujenga uwezo wa wadau wa tasnia ya ujenzi, kukuza weledi katika usimamizi wa mikataba na kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro, ili kuhakikisha miradi ya ujenzi inatekelezwa kwa ufanisi na kuchangia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.