USIMAMIZI WA GHARAMA KULINDA MIRADI YA UJENZI

USIMAMIZI WA GHARAMA KULINDA MIRADI YA UJENZI

02 Nov, 2026
USIMAMIZI WA GHARAMA KULINDA MIRADI YA UJENZI

Usimamizi sahihi wa mabadiliko ya gharama katika mikataba ya ujenzi unaweza kulinda fedha za umma, kupunguza migogoro na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati kwa ajili ya manufaa ya wananchi.

Hayo yamebainishwa katika mafunzo ya namna ya kukabiliana na mabadiliko au marekebisho ya bei katika mikataba ya ujenzi (Practicability of Price Adjustment in Construction Contracts), yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) mkoani Morogoro, kuanzia Oktoba 26 hadi 30, 2026.

Mkufunzi wa mafunzo hayo ,Dkt. Leonard Chamuriho, amesisitiza kuwa maamuzi ya kuongeza gharama lazima yawe na msingi unaoweza kuthibitishwa. “Kabla ya kuidhinisha ongezeko lolote la gharama, tunapaswa kujiuliza: ni tukio gani lilisababisha ongezeko hilo, ni kifungu gani cha mkataba kilichosainiwa kinaunga mkono suluhisho, na je, mtu mwingine anaweza kurudia hesabu hizo na kufikia matokeo yaleyale? Si kila ongezeko la gharama linatoa moja kwa moja ruhusa ya kuongeza bei ya mkataba,” amesema.

Naye ,Bi. Isabella Alex, wakili wa serikali kutoka Ofisi ya wakili mkuu wa serikali, ambae ni mmoja wa washiriki wa Mafunzo hayo amesema amepata uelewa juu ya umuhimu wa kuzingatia masharti ya mkataba na kutumia taratibu sahihi katika maamuzi.

Kupitia mafunzo hayo, NCC inaendelea kutimiza dhamira yake ya kuimarisha na kukuza uwezo wa wadau wa sekta ya ujenzi na kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa tija, kwa kuwa miundombinu imara na yenye gharama zinazodhibitiwa ni nguzo ya kufikia maendeleo yaliyokusudiwa katika Dira ya Taifa 2050.