Historia Fupi

Historia Fupi

Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) lilianzishwa mwaka 1979 kupitia Sheria ya Bunge Na. 20 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake tarehe 17 Agosti 1981 kupitia Tangazo la Serikali Na. 95 la mwaka 1981. Mwaka 2007, sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Bunge Na. 25 ya mwaka 2007, kama ilivyorejewa katika Toleo Lililorekebishwa la Sura ya 162 la mwaka 2008. Kuanzishwa kwa Baraza hili kulikuwa hatua muhimu iliyolenga kukuza maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini Tanzania, na pia kuonesha kutambuliwa kwa umuhimu wa kimkakati wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa taifa kwa ujumla. Kabla ya kuanzishwa kwa NCC, sekta ya ujenzi ilikuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zilizoipelekea Serikali kufanya utafiti kuhusu sekta hiyo mwaka 1976.

Lengo la utafiti huo lilikuwa kubaini sababu zilizochangia hali isiyoridhisha ya sekta ya ujenzi na kupendekeza hatua stahiki za kuboresha hali hiyo. Utafiti huo ulibaini kuwepo kwa matatizo na mapungufu mbalimbali yaliyoathiri maendeleo na utendaji wa sekta hiyo. Miongoni mwa changamoto zilizobainika ni ukosefu wa uratibu ndani ya sekta, hali iliyosababisha taasisi nyingi kufanya kazi kwa kujitegemea bila kuwa na taarifa sahihi kuhusu shughuli zinazofanywa na taasisi nyingine.

Aidha, kulikuwa na mwingiliano wa majukumu na matumizi yasiyo bora ya rasilimali chache za taifa, jambo lililoathiri utekelezaji mzuri wa programu za sekta hiyo. Mazingira yasiyopangwa na yasiyoratibiwa vizuri pia yalionekana kuwa na athari hasi katika matumizi na maendeleo ya rasilimali watu. Vivyo hivyo, upatikanaji wa vifaa vya ujenzi, mawasiliano, mipangilio ya kazi na ufanisi kwa ujumla uliathirika.

Kutokana na hali hiyo, ilionekana kuwa ni muhimu kuwepo kwa mfumo wa kukusanya na kuchapisha taarifa za sekta, pamoja na kuratibu na kupanga mikakati ya kuboresha utendaji na ukuaji wa sekta ya ujenzi. Hivyo, utafiti huo ulipendekeza kuanzishwa kwa Baraza la Ujenzi ambalo lingepewa jukumu la kuratibu na kuhamasisha maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini Tanzania. Aidha, Baraza hilo lilitakiwa kuongoza utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyotolewa na utafiti huo.