Kaguzi za kiufundi

Kaguzi za kiufundi

27 May, 2026
Kaguzi za kiufundi

Ubora wa mradi haupaswi kubahatishwa.

Iwe ni jengo, barabara, daraja, mradi wa maji, mashine, mitambo au mifumo mbalimbali, huduma za Ukaguzi wa Kiufundi za Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) zinakupa uhakika kwamba kazi inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, mahitaji ya kiufundi na matumizi yaliyokusudiwa.

Kwa kutumia timu ya wataalamu wenye uzoefu katika nyanja mbalimbali za uhandisi na teknolojia, NCC hutoa tathmini  ya kitaalamu inayosaidia kubaini mapema changamoto, kuongeza ubora wa utekelezaji na kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali katika miradi ya maendeleo.

Ukaguzi wa Kiufundi ni Nini?

Ukaguzi wa Kiufundi ni uchunguzi au tathmini ya kitaalamu unaofanywa ili kuhakikisha kuwa vifaa, mifumo, majengo, mashine au kazi za ujenzi zinakidhi viwango, kanuni na mahitaji ya kiufundi yaliyowekwa.

Huduma hii husaidia kuthibitisha ubora wa utekelezaji wa mradi, kubaini mapungufu yanayoweza kujitokeza na kutoa mapendekezo ya kitaalamu yanayosaidia kuboresha utekelezaji wa kazi kabla changamoto hazijaleta athari kubwa.

Tunakagua Nini?

Huduma zetu zinahusisha ukaguzi wa miradi na mifumo mbalimbali.

NCC hufanya ukaguzi wa kiufundi wa:

  • Majengo
  • Barabara
  • Madaraja
  • Miradi ya maji
  • Miundombinu mingine ya ujenzi
  • Mashine
  • Mitambo
  • Vifaa mbalimbali
  • Mifumo mbalimbali

Aidha, kutokana na kuwa na wataalamu wenye ujuzi na uzoefu katika taaluma mbalimbali za uhandisi na teknolojia, NCC ina uwezo wa kufanya ukaguzi wa aina mbalimbali za ununuzi ili kuhakikisha bidhaa, vifaa na mifumo vinakidhi viwango vya ubora, mahitaji ya kiufundi na matumizi yaliyokusudiwa.

Ukaguzi Hufanyika hatua gani ya ujenzi?

Hakuna wakati mmoja sahihi ukaguzi hufanyika pale unapohitajika.

Ukaguzi wa Kiufundi unaweza kufanyika katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi kulingana na mahitaji ya mradi husika au maamuzi ya mtekelezaji wa mradi yanayotokana na tathmini ya vihatarishi (Risk Assessment).

Kwa Nini Uchague Huduma za Ukaguzi wa Kiufundi wa NCC?

Kupitia huduma za Ukaguzi wa Kiufundi, NCC husaidia:

  • Kuhakikisha miradi inazingatia viwango vya ubora.
  • Kubaini kasoro na mapungufu mapema.
  • Kuongeza usalama wa miradi.
  • Kusaidia kufanya maamuzi ya kiufundi na kiutendaji.
  • Kuboresha matumizi ya rasilimali na thamani ya fedha.
  • Kutoa mapendekezo ya maboresho yanayotekelezeka.

Jinsi ya Kuomba Huduma

Ni rahisi kuanza.

Unaweza kuomba huduma za Ukaguzi wa Kiufundi kwa njia mbili:

1. Barua Rasmi

Wasilisha barua ya maombi kwa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC). Endapo itahitajika, unaweza pia kuomba NCC kuandaa pendekezo la kitaalamu (Technical Proposal).

Ili kurahisisha maandalizi ya pendekezo hilo, inashauriwa kuambatanisha Hadidu za Rejea (Terms of Reference – ToR) zinazoeleza upeo wa kazi inayokusudiwa kufanyiwa ukaguzi.

2. Kupitia Mfumo wa NeST

NCC pia imesajiliwa katika Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) hivyo mteja anaweza kutangaza zabuni au kuomba mapendekezo kupitia mfumo huo, ambapo NCC inaweza kushiriki kama mzabuni au kupitia utaratibu wa Serikali kwa Serikali (Government-to-Government – G2G) pale sheria na taratibu zinaporuhusu.

Gharama za Huduma

Kila mradi ni wa kipekee. Hivyo ndivyo ilivyo pia kwa gharama za ukaguzi.

Ada za huduma za Ukaguzi wa Kiufundi hutegemea mahitaji ya kazi husika. Miongoni mwa mambo yanayozingatiwa ni: Aina ya ukaguzi unaohitajika, upeo wa kazi, idadi ya maeneo au miradi, eneo la kijiografia, idadi na taaluma za wataalamu, muda wa utekelezaji, ugumu wa kazi na rasilimali zinazohitajika.

Baada ya kupokea maombi yako, NCC huandaa Technical and Financial Proposal inayobainisha mawanda ya kazi, mbinu za utekelezaji, muda na gharama za huduma.