Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) linatarajia kuandaa Kongamano la Wadau wa Sekta ya Ujenzi (Construction Industry Forum), litakalowakutanisha wadau mbalimbali wa tasnia ya ujenzi kwa lengo la kukuza uwezo, kubadilishana uzoefu na kuongeza tija katika sekta hiyo.
Hayo yameelezwa Leo jijini Dodoma, katika Kikao cha 112 cha Bodi ya NCC kilichowakutanisha Wajumbe wa Bodi na Wakuu wa Vitengo, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Fatma Mohamed.
Kikao hicho kimejadili tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza, ikiwemo kukuza na kuendeleza sekta ya ujenzi, kutoa ushauri wa kitaalamu, kujenga uwezo wa wadau kupitia mafunzo, kufanya tafiti, pamoja na kusaidia utatuzi wa migogoro katika miradi ya ujenzi.
Kuandaa makongamano na warsha zinazowakutanisha wadau ni moja ya majukumu ya msingi ya NCC hivyo, Kupitia kongamano hilo, wakandarasi, wataalamu, wamiliki wa miradi, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wengine watapata jukwaa la pamoja la kujadili changamoto, fursa na mwelekeo wa tasnia ya ujenzi nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Fatma Mohamed amesema,
"Sekta ya ujenzi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa letu, Kongamano la Ujenzi litakuwa jukwaa muhimu la kuwaleta wadau pamoja, kujenga uwezo wao na kuhakikisha huduma za Baraza zinaleta tija halisi kwa kila mkandarasi, mtaalamu na mmiliki wa mradi wa ujenzi."
Kwa upande wao, Wajumbe wa Bodi wametoa michango mbalimbali, wakisisitiza maandalizi ya kongamano hilo kuanza mapema pamoja na kuwashirikisha kikamilifu wadau wa sekta ya ujenzi katika hatua zote, ili kuhakikisha kongamano linajibu mahitaji halisi ya tasnia na kuleta matokeo yenye tija.
Naye Mtendaji Mkuu wa NCC, Dkt. Matiko Mturi, ambaye pia ni Katibu wa Bodi, amepokea maelekezo ya Bodi na kuahidi kuyasimamia kwa ajili ya utekelezaji kwa kasi zaidi, ili malengo ya Baraza na matarajio ya wadau wa sekta ya ujenzi yafikiwe kwa wakati.
Kikao hiki ni sehemu ya jitihada endelevu za NCC katika kuhakikisha uwajibikaji, uwazi na usimamizi madhubuti wa mipango ya Baraza, ili sekta ya ujenzi iendelee kuchangia ipasavyo katika ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa ajira na ujenzi wa miundombinu bora na salama nchini.