Tutazingatia maadili ya Utumishi wa Umma-NCC

News Image Dec, 17 2020

MAOFISA wanaoshughulika na masuala ya maadili ya Utumishi wa Umma kutoka Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora) wametoa mafunzo ya maadili kwa wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) jana na kuwakumbusha mambo muhimu wanayopaswa kuyazingatia.

Mafunzo hayo ya siku moja yalitolewa katika Makao Makuu ya NCC yaliyopo ghorofa ya Tisa, Mtaa wa Mansfield, Dar es Salaam chini ya Usimamizi wa Mkurugenzi Msaidizi anayehusika na Ufuatiliaji uzingatiaji wa Maadili ya Utumishi wa Umma katika taasisi mbalimbali za Umma nchini, Janet Mishinga.

Katika mafunzo hayo yaliyotolewa kwa ushirikiano wa Ofisa Utumishi Mwandamizi kutoka Ofisi hiyo ya Rais, Margareth Ngondya, wafanyakazi wa NCC walikumbushwa vipengele muhimu vya kuzingatia ili kuhakikisha mafanikio katika utendaji wao mahali pa kazi, ikiwemo kuepuka uzinzi, uasherati, rushwa, pamoja na zawadi zenye thamani inayozidi Sh 200,000/=.

Akizungumzia miongozo mbalimbali ya Serikali inayotolewa katika taasisi za Umma, Mishinga alisema, ni vyema ikafuatwa ili kuepuka migongano inayoweza kusababisha watumishi kuvunja sheria na taratibu katika utendaji wa kazi.

Aidha, alisema miongozo, sheria na taratibu za utendaji katika Utumishi wa Umma hazipaswi kuchukuliwa kama kitu kibaya au tatizo kwa sababu inasaidia kuelekeza jinsi kazi zinavyopaswa kufanywa kwa namna inayofaa.

“Ukiona mtumishi anachukia miongozo ujue huyo ana mambo yake ya tofauti na yanayotakiwa katika Utumishi wa Umma. Mara nyingi watumishi wa aina hiyo wanakuwa si waadilifu, tujitahidi kufuata taratibu kuanzia kwenye mavazi hadi namna ya kushughulikia masuala ya watumishi wenzetu, kwa wale walio katika nafasi za uongozi”alisema Mkurugenzi Msaidizi huyo.

Katika hatua nyingine, viongozi wa NCC walikumbushwa kuwa makini wakati wa kusikiliza malalamiko ya wateja kwa kuhakikisha wanasikiliza pande zote na kujiridhisha kabla ya kutoa uamuzi.

Ngondya aliyehusika kutoa mafunzo kuhusu eneo la malalamiko alisema si wakati wote watumishi wa Umma katika taasisi Fulani Fulani za Umma wanaolalamikiwa ndio wenye matatizo.

Alisema, “Wakati mwingine wateja wanakuwa na matatizo na wanawahi kulalamika kwa viongozi wa taasisi, katika suala kama hili ni vyema pande zote zikasikilizwa na si walalamikaji wan je pekee ili kuepusha kutowatendea haki watumishi wanaolalamikiwa”.

Katika mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa NCC, Dk. Matiko Mturi aliahidi kuhakikisha maadili yanazingatiwa na wafanyakazi wote na kwamba wao wakiwa ndio menejimenti, watahakikisha kutakuwa na hatua mbalimbali za kukumbushana mambo muhimu ili sheria zisivunjwe.