NCC yashiriki maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani

WATUMISHI wanawake wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), wameungana na wanawake wenzao duniani kusherehekea siku yao, iliyolenga kusisitiza haki, usawa na uwezeshaji kwa wasichana na wanawake.
Kwa mkoa wa Dodoma maadhimisho hayo yameanza kwa maandamano kutoka eneo la Nyerere ‘Squre’, katikati ya jiji, na kukamilishwa kwenye viwanja vya Chinangali.
Katika maadhimisho hayo, mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Alhaj Jabir Shekimweri aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewataka wanawake watumie ipasavyo fursa za kiuchumi wanazozipata, ili kuleta maendeleo.
Amesema, wanawake wana sifa ya uaminifu na si ubadhirifu, hivyo, wana uwezo wa kusababisha maendeleo wanapotumia vyema fursa za kiuchumi wanazozipata.
“Kwa sababu hiyo, natoa wito kwa jamii na wadau wa maendeleo nchini, kutoa fursa za kutosha na haki sawa kwa wanawake kushiriki kujenga uchumi wa nchi,”amesema.
Ameongeza kuwa, kuwekeza kwa mwanamke na msichana ni kuwekeza kwa maendeleo ya jamii nzima na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mhe. Jabir amewataka wanawake na wasichana nchini kutumia vizuri fursa za elimu wanazozipata ili kujiendeleza katika masuala mbalimbali, ikiwemo teknolojia. Amesema kumuelimisha mwanamke na msichana ni kuielimisha jamii.
Maadhimisho hayo yenye Kauli Mbiu isemayo Wanawake na Wasichana tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji, yamepambwa na ngoma kutoka vikundi mbalimbali, maonesho ya kazi za wanawake wajasiriamali, ikiwemo bidhaa wanazotengeneza kwa ajili ya biashara.
Pia, simulizi zenye kutia hamasa na ushawishi wa kujitafutia maendeleo zimetolewa na wanawake wenye mafanikio waliojumuika kwenye maadhimisho hayo zikiwa kama darasa lenye msukumo wa ‘kuchangamkia fursa’ za kujiendeleza kwa wanaozipata.