NCC YAFUNZA MBINU BORA ZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA...

NCC YAFUNZA MBINU BORA ZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UJENZI

19 Jun, 2026
NCC YAFUNZA MBINU BORA ZA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UJENZI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) imeendelea kuimarisha sekta ya ujenzi nchini kwa kuwajengea uwezo wadau mbalimbali wa ujenzi kupitia mafunzo ya usimamizi wa mabadiliko ya bei katika mikataba ya ujenzi.

Mafunzo hayo yamekusudia kuongeza ufanisi wa usimamizi wa miradi na kupunguza migogoro ya kimkataba inayotokana na mabadiliko ya gharama za ujenzi.

Akizungumza jijini Arusha wakati wa mafunzo hayo, Mhandisi, Dkt. Leonard Madaraka Chamuriho ambae ni mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo amesema, mafunzo hayo yamelenga kuhakikisha wadau wa sekta ya ujenzi wana ufahamu wa jinsi ya kushughulikia mabadiliko ya gharama katika miradi ya ujenzi na kuendana na mabadiliko ya soko katika hatua zote za miradi ya ujenzi.
" Changamoto hizi ambazo zinatokana na mabadiliko ya bei kama vile kupanda kwa bei ya mafuta,ambalo sio kosa la mwenye mradi wala sio kosa la mkandarasi inabidi kuwe na utaratibu wa kimkataba wa kushughulikia mabadiliko hayo…

Kwahiyo inabidi tuweke utaratibu mzuri na wadau wote waelewe ili kusiwe na malalamiko ya mtu kupunjwa au kuibiwa" amesema Dkt. Chamuriho.

Aidha, ameeleza kuwa mafunzo yanayotolewa na NCC ni muhimu kwa wadau wote wa sekta ya ujenzi kushiriki kwa sababu yanatoa uelewa mzuri kwenye maeneo yote ambayo yanaonekana yana changamoto katika sekta ya ujenzi.

“Baraza la Taifa la Ujenzi lina jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba sekta hii ya ujenzi inakwenda kama inavyotakiwa,na kwa kutoa mafunzo haya inatoa uelewa mzuri kwa maeneo yote yenye changamoto ,kwa mfano hili la mabadiliko ya bei yanayosabishwa na mabadiliko katika soko, vita au majanga ya asili.” ameongeza.

Kwa upande wa washiriki,Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Pascas Alexander Masoye, amesema mafunzo haya yameendelea kuwakumbusha mambo muhimu yanayotakiwa kufuatwa kwenye miradi ya ujenzi ili kuepusha migogoro inayotokea wakati wa utekelezaji wa miradi.

“mafunzo haya yameendelea kwanza kutukumbusha namna bora ya kusimamia ama ya kuchagua indices kabla ya kuingia kwenye mkataba ili muhakikishe kuwa mnachokichagua mmekubaliana wote na pia kipo reliable”amesema

Mhandisi kutoka Wizara ya UJenzi na Uchukuzi kutoka visiwani Zanzibar, mha.Samira Abubakar Mohamed,amesema mafunzo haya yamewapa maarifa ya kuweka kumbukumbu juu ya mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza katika mikataba.

“maarifa ambayo nimejifunza ambayo ni muhimu zaidi ni namna nzur zaidi ya uwekaji kumbukumbu wakati tunapo manage mikataba yetu kwa sababu kumbukumbu nzuri zinatusaidia hata tukikutana na changamoto kama vile mabadiliko ya bei na kujua lini mambo haya yalibadilika” amesema.

Naye, Mratibu msaidizi wa miradi ya ufadhili wa Benki ya Dunia kutoka TARURA,Mha.Lwitiko Joel Mwandobo,ameiomba NCC kuendelea kuandaa mafunzo mbalimbali kwa wadau wa sekta ya ujenzi kwenye maeneo mbalimbali kama vile uandaaji wa mikataba ,usimamizi wa mikataba na pia namna ya kushughulikia migogoro inayojitokeza kwenye mikataba ya ujenzi ili miradi iweze kukamilika vizuri.

Kupitia mafunzo hayo, washiriki wamepata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za kushughulikia masuala ya mabadiliko ya bei katika mikataba ya ujenzi kwa kuzingatia misingi ya kitaalamu, sheria na taratibu zinazotumika katika sekta hiyo.