Sekta ya Ujenzi ni moja ya nguzo muhimu za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kutambua hilo Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limeendelea na mchakato wa kuboresha sheria ya NCC ili kuendana na mahitaji ya sasa ya maendeleo, mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya teknolojia katika sekta ya Ujenzi nchini.
Akifungua kikao cha wadau wa sekta ya ujenzi kilicholenga kukusanya maoni na mapendekezo kuhusu marekebisho ya sheria ya NCC, Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Dkt. Matiko Mturi, amesema maboresho hayo yanakusudia kuhakikisha sekta ya ujenzi inaendana na kasi ya maendeleo ya nchi na mahitaji ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ameeleza kuwa marekebisho hayo ya sheria ya NCC, ni jambo la kizalendo na lenye kuleta maendeleo nchini, hivyo kila mtu ana wajibu wa kutoa maoni na mapendekezo ili kuweza kuboresha sekta ya ujenzi nchini.
“Hili jambo tunalolifanya ni la kizalendo na lenye kutamani kuiona Tanzania ambayo tunaitaka, huko zamani tulikuwa tunaambiwa watu walipigania uhuru au unaweza ukasoma unaona mtu fulani alitoa mchango katika maendeleo ya nchi fulani na wewe ukadhani huwezi kutoa mchango, fursa ni kama hizi za kutoa mchango, maoni, mapendekezo ya nini kifanywe ili kuboresha taasisi yenye kutumia fedha za umma kwa ajili ya mendeleo ya Umma” amesema Dkt. Mturi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tafiti na Maendeleo wa NCC, Mhandisi Anselim Kiseku, amesema marekebisho ya sheria yanatarajiwa kuongeza uwezo wa Baraza kusimamia sekta ya ujenzi kwa ufanisi zaidi, kupitia kuimarisha udhibiti wa ubora wa kazi za ujenzi, usimamizi wa taarifa za miradi na uwajibikaji wa wadau wa sekta hiyo.
“Tunategemea tukifanya marekebisho haya Baraza litaimarika sana na litaweza sasa kusimamia tasnia ya ujenzi vizuri, kuimarisha udhibiti wa ubora wa kazi za majenzi hapa nchini lakini kusimamia sekta ndogo ya majengo, kuwepo kwa mfumo wa utunzaji wa orodha na taarifa za miradi ya majenzi, Pamoja na kuongeza uwajibikaji wa wadau wa tasnia ya ujenzi” amesema

Akichangia mjadala huo, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Nishati, Eliasi Nawera, ameipongeza NCC kwa kuendelea kuchukua hatua za kuboresha mifumo na sheria zinazosimamia sekta hiyo, ameeleza kuwa jitihada hizo zina mchango mkubwa katika kuimarisha utendaji wa sekta ya ujenzi nchini.

Naye Mkadiriaji Majenzi kutoka TARURA, Joshua Tenga, amesema marekebisho ya sheria ya NCC yana umuhimu mkubwa katika kuiwezesha sekta ya ujenzi kuchangia kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kukuza uchumi wa taifa.
Kupitia kikao hicho, wadau kutoka wizara na taasisi mbalimbali walipata fursa ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo yatakayosaidia kuiboresha sheria ya NCC ili marekebisho hayo yakidhi matarajio ya sekta na kuchangia kikamilifu safari ya Tanzania kuelekea Dira ya Taifa na maendeleo ya 2050.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Baraza la Taifa la Ujenzi (N...
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amewataka wakandarasi nchini kutekeleza m...
Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limesema uwezekano wa migogoro ya kib...
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe...
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe...