NCC -TAMICO yapata viongozi

News Image Nov, 12 2020


CHAMA cha Wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC-TAMICO) kimepata viongozi wapya wiki hii,baada ya waliokuwa wakikiongoza kumaliza muda wao wa uongozi.

Uchaguzi huo wa Mwenyekiti na Katibu wa NCC- TAMICO, Mwenyekiti na Katibu wa NCC-TAMICO Wanawake, pamoja na NCC-TAMICO Vijana, ulihusisha wanachama wa chama hicho katika tawi la NCC pekee.

Uchaguzi ulifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa NCC, uliopo Ghorofa ya 9 katika jengo la Samora (Samora Tower), Mtaa wa Mansfield, Dar es Salaam, na kusimamiwa na Katibu wa TAMICO kutoka wilayani Ilala, Dar es Salaam, Bi. Grace Mkella.

Waliochaguliwa na nafasi zao katika mabano ni Godbless Mwanri (Mwenyekiti-NCC -TAMICO), Zephania Laiser (Katibu NCC -TAMICO), Bertha Musa ( Mwenyekiti NCC-TAMICO WANAWAKE) na Emma Mchome (Katibu NCC-TAMICO WANAWAKE) .

Wengine waliochaguliwa ni Anitha Malewo ( NCC-TAMICO VIJANA) na Katibu wake Victor Mtae. Mbali na hao, walichaguliwa wajumbe wa kamati mbalimbali zilizo kwenye mabano, akiwemo Monica Mahani (Mjumbe Kamati ya Wanawake) na Ruth Mndenye (Mjumbe Kamati ya Wanawake). Wengine ni wajumbe wa Kamati ya Vijana; Dorine Silayo na Mohammed Mhina.

Kwa mujibu wa Katibu wa NCC-TAMICO aliyemaliza muda wake, Ramadhani Matenga, katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wao, 2015 hadi 2020 walifanikiwa kuanzisha Baraza la Wafanyakazi na Mkataba wa kutambuana kati ya NCC na TAMICO.

“Pia, tumefanikiwa kuandaa Mkataba wa Hali Bora na kuukabidhi kwa menejimenti, ili ufanyiwe kazi na kuridhiwa. Bado haujarejeshwa kwa chama, hivyo tunaendelea kuvuta subira tukiamini kuwa wenzetu waliochaguliwa sasa wataendelea nao ukiwa umekamilishwa,”Matenga anasema.

Kwa maelezo ya Matenga, uchaguzi mwingine utafanyika mwaka 2025. Aidha, alisema wana matarajio kuwa Chama cha Wafanyakazi katika NCC kitakua zaidi, kwa sababu waajiriwa wapya wanaendelea kuletwa kwenye baraza hilo kila siku.

Kwa upande wake, Mwanri alisema watahakikisha ushirikiano uliokuwepo kati ya wafanyakazi, hususan wana chama wa TAMICO na menejimenti unaendelea kudumu, ili malengo ya taasisi yafikiwe.

Aliongeza kuwa nchi yetu ni ya uchumi wa kati, hivyo watahakikisha wafanyakazi wanawajibika ipasavyo katika majukumu yao kiasi cha kuendana na matakwa ya kuukuza uchumi huo wa kati.

Wakati huo huo, Katibu mpya wa NCC-TAMICO, Zephania Laizer alisema anaamini katika ushirikiano, hivyo, atahakikisha anakuwa kiungo bora kati ya menejimenti ya NCC na wafanyakazi wa taasisi hiyo ambao ni wanachama wa TAMICO, kwa maslahi ya taifa.