NCC Hazina Saccos yapata viongozi

News Image Oct, 12 2020

CHAMA cha Kuweka na Kukopa kwa ajili ya watumishi wa Serikali wanaofanya kazi kwenye Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC Hazina Saccos), kimepata viongozi baada ya kufanyika uchaguzi kwenye tawi hilo hivi karibuni.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 08, mwaka huu kwenye ukumbi mdogo wa mikutano wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), lililopo mtaa wa Mansfield jijini Dar es Salaam, walichaguliwa Mwenyekiti, Katibu na Mweka Hazina.

Viongozi kutoka Makao Makuu ya Hazina Saccos ndio walio ratibu na kusimamia uchaguzi huo ambao pia ulihudhuriwa na Mtendaji Mkuu wa NCC, Dk. Matiko Mturi, aliyekuwa mfano bora wa kuigwa kwenye mkutano huo, kutokana na kuuliza maswali mbalimbali ya msingi kuhusu mambo tofauti ya maslahi ya wanachama, kwa manufaa ya wote waliojiunga na chama hicho.

Mara baada ya wanachama kuelekezwa masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na kujibiwa maswali waliyouliza, uchaguzi ulifanyika na kupatikana Mwenyekiti ambaye ni Bw. Godbless Mwanri (Pichani), Katibu Bi. Emma Mchome na Mweka Hazina Bw.Tumaini Masige.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Mwenyekiti wa NCC Hazina Saccos, Bw. Mwanri alisema watakuwa madarakani kwa muda wa miaka mitatu kama Katiba ya chama inavyoelekeza.

“Tunachoahidi ni kutoa ushirikiano kwa wanachama wote. Lengo letu la msingi ni kuhakikisha kuwa NCC Hazina Saccos inakuwa ya manufaa kwa kila mwanachama kwa kutoa huduma inayo kusudiwa kwa muda unaotakiwa,”.

Mbali na uchaguzi wa viongozi hao, watumishi wa NCC waliojiunga na baraza hilo hivi karibuni ambao si wanachama wa Saccos hiyo walipewa nafasi wajiunge, kwa kila aliyetaka na kukabidhiwa fomu za uanachama.

Kwa mujibu wa Bw. Mwanri, NCC imejiunga na Hazina Saccos Mei, mwaka huu na ina mpango wa kuhakikisha wanapatikana wanachama wengi zaidi watakaojiunga kutokana na juhudi waliyopanga kuifanya viongozi hao kuhakikisha malengo mazuri, mipango na faida za chama zinaelezwa kwa ufasaha kwa kila asiye mwanachama, ili aone umuhimu na kujiunga.

“Saccos zinasaidia sana hasa hii ya Hazina ambayo makato yake si ya kuumiza ‘kivile’, tofauti na nyingine tulizowahi kuzifahamu. Kwa mwajiriwa anayependa kujiunga nafasi zipo na fomu zipo, cha msingi ni kufuata viongozi ili kuelekezwa nini cha kufanya,”anaeleza Bi. Mchome.