NAIBU WAZIRI UJENZI AZINDUA BARAZA LA WAFANYAKAZI LA BARAZA LA TAIFA LA UJENZI (NCC)
Oct, 24 2024Dodoma, Oktoba 23, 2024
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Godfrey Msongwe Kasekenya (Mb.), amezindua Baraza la Wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mabeyo, jijini Dodoma.
Mhe. Kasekenya amepongeza menejimenti ya NCC kwa kutekeleza maagizo ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, kuhusu kuundwa kwa Baraza la Wafanyakazi. Ameeleza kuwa hatua hii inaashiria dhamira ya taasisi hiyo katika kuboresha utendaji wake kwa manufaa ya wafanyakazi na taifa kwa ujumla.
Wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi, Mhe. Kasekenya amesema kuwa “Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu linalosaidia kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya menejimenti na wafanyakazi. Kupitia baraza hili, masuala muhimu kama mipango ya taasisi, bajeti, na utendaji wa kazi yanaweza kujadiliwa kwa pamoja ili kufikia malengo ya taasisi na kuboresha mazingira ya kazi,”
Aidha, Naibu Waziri amewasihi wajumbe wa baraza hilo kutumia kikamilifu nafasi yao ya uwakilishi kwa kuwasilisha kwa ufanisi masuala yanayowahusu wafanyakazi. Amesisitiza umuhimu wa kutumia baraza kujadili changamoto na kutoa mapendekezo chanya yatakayosaidia kuboresha utendaji wa NCC. Katika hotuba yake, Mhe. Kasekenya pia amehimiza uwajibikaji, maadili kazini kuepuka vitendo vya rushwa, matumizi yasiyifaa ya rasilimali za ummapamoja na matumizi mabaya ya madaraka.
Akihitimisha Mhe. Kasekenya ameeleza nia yake ya kuendelea kushirikiana na viongozi wa wizara ili kuhakikisha NCC inatekeleza majukumu yake kikamilifu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NCC, Arch. Dkt. Fatma Mohammed, ameeleza umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi katika kuhakikisha mazingira mazuri ya kazi na uhusiano imara kati ya wafanyakazi na menejimenti.
“Uwepo wa Baraza la Wafanyakazi utatoa fursa kwa wafanyakazi na menejimenti kujadili masuala ambayo hayajapatiwa ufumbuzi katika ngazi nyingine na kusaidia kujenga mazingira bora ya kazi kwa utendaji bora zaidi,”amesema Dr. Mohammed.
Dkt. Mohammed pia ametilia mkazo jukumu muhimu la NCC katika kuratibu sekta ya ujenzi nchini, na kusisitiza mahusiano mazuri ya ndani na ushirikiano na wadau ni muhimu ili kufanikisha malengo ya taasisi hiyo.