Muongozo bora kusimamia mikataba ya ujenzi wa barabara waandaliwa

BARAZA la Taifa la Ujenzi (NCC) linaandaa muongozo wa usimamizi wa mikataba ya ujenzi wa barabara nchini, kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya barabara yenye ubora unaoendana na thamani ya fedha zinazotumika kuitekeleza, lengo likiwa kuongeza tija na ufanisi.
Muongozo huo utaisaidia TANROADS kuwa na usimamizi mzuri zaidi wa mikataba ya ujenzi wa barabara katika hatua zote za miradi zinazoanzia kwenye maandalizi na utekelezaji.
Wataalamu wanaouandaa wamesema kwa nyakati tofauti wakati wa maandalizi ya muongozo huo jijini Arusha kuwa unaleta usawazishaji unaoainisha viwango vinavyokubalika katika utekelezaji wa miradi ya barabara, ili vifuatwe na kuzingatiwa wakati wote wa usimamizi wa mikataba ya ujenzi wa barabara nchini.
Amesema nyakati hizo ni pamoja na za maandalizi na utekelezaji wa miradi husika ya barabara, lengo likiwa kuleta matokeo chanya yanayokusudiwa.
Kwa mujibu wake, mungozo huo unagusa maeneo mbalimbali, baadhi yakiwa ni mipango, afya na usalama, mawasiliano yenye mrejesho, vifaa, usimamizi wa ubora, mazingira, usimamizi wa uhusiano mwema na wadau wa barabara, kuzuia migogoro na usuluhishi, uwekaji na utunzaji wa taarifa za mradi au miradi husika inayotekelezwa, pamoja na utoaji wa ripoti za mradi au miradi hiyo, hasa wakati wa usimamizi wake.
“Kupitia muongozo huu tunaouandaa na kwa kuzingatia vipengele vyote vinavyoboreshwa, tutaweza kuleta ufanisi kwa kurahisisha usimamizi wake kwenye maeneo tofauti ya ujenzi wa miradi ya barabara zetu. Aidha, masuala kama gharama zisizo za lazima zinazoongezeka, migogoro na mengine yanayojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ya barabara yataweza kuepukwa,” Mha. Nnko anasema na kusisitiza kuwa kwa kadri utakavyokuwa ukitumika, muongozo huo utaendelea kuboreshwa.
Muongozo huo unaainisha nini?
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NCC, Mha. Dkt. Matiko Mturi, ameeleza kuwa muongozo huo utaainisha kwa kina masuala muhimu mbalimbali yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa usimamizi wa mikataba ya ujenzi wa barabara, zikiwemo njia bora na taratibu zinazopasa kutumika, lengo likiwa kuleta tija kwa kuhakikisha ubora unaokusudiwa katika utekelezaji wa ujenzi wa barabara nchini ziendane na thamani halisi ya gharama zinazotumika.
Amesema muongozo huo utakuwa ni zana muhimu na bora. Ameongeza,:”Ukitumiwa vizuri, utaleta matokeo chanya. Tunategemea hili liwezekane kwa kuhakikisha mafunzo kwa watumiaji kwaza ili wauelewe na kujua namna ya kuutumia kwa usahihi”.
Neno kutoka kwa wataalamu wa NCC
Wakati huo huo, Mha. Tumaini Lemunge anayeongoza wataalamu wanaoandaa muongozo huo kutoka NCC amesema kwa niaba ya wenzake kuwa walifanya utafiti wa kina kuhusu miongozo iliyopo na kubaini kuwepo kwa mapungufu yaliyohitaji kuondolewa.
Kwa maoni yao, muongozo huo ukikamilika na kutumiwa ipasavyo, utaziwezesha taasisi zinazohusika na masuala ya usimamizi wa miradi ya barabara zote kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa tija, hivyo kuleta ufanisi.
Pamoja na majukumu mengine, NCC inaishauri Serikali kuhusu masuala mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Ujenzi nchini, ikiwa ni pamoja na kuandaa au kuboresha miongozo kwa ajili ya sekta hiyo.