Bashungwa: Wakandarasi Wazawa Washirikishwe Fursa za Kiuchumi
Oct, 02 2023Serikali imezitaka taasisi chini ya Wizara ya Ujenzi kuhakikisha Wakandarasi Wazawa wanapewa kipaumbele katika kushiriki kwenye fursa za kiuchumi.
Maagaizo hayo yametolewa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) jijini Dodoma alipokutana na kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu ya taasisi nne za Wizara hiyo ambazo ni Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).
Mhe. Bashungwa alisema, inafaa sasa kuwepo na jitihada za makusudi na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Makandarasi Wazawa wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya Sekta ya Ujenzi nchini ili kuleta tija kwa Makandarasi hao na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Waziri Bashungwa alizitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi kukaa na kusikiliza changamoto zinazowakabili wadau wa sekta ya ujenzi na kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kuandaa mikakati itakayosaidia wakandarasi hao kutekeleza miradi mingi hasa ya kimkakati itakayoweza kuinua mitaji yao.
“Linapokuja suala la ‘Local content’ yaani fursa za kiuchumi kwa watanzania, Mheshimiwa Rais kiu yake ni kuona ushiriki wa Makandarasi wazawa kwenye maendeleo ya Sekta ya Ujenzi unaongezeka”, amesema Mhe. Bashungwa.
Waziri Bashungwa ameeleza kuwa Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa idadi ya Wakandarasi waliosajiliwa na Bodi ni 14,550 ambapo kati ya hao 550 ni Wakandarasi wa nje na 14,000 ni Wakandarasi wazawa lakini katika utekelezaji wa miradi Wakandarasi wazawa wanapata asilimia 54 na Makandarasi wa nje wanapata asilimia 46 ya miradi iliyotekelezwa.
Aidha, Waziri Bashungwa ameishukuru Serikali kupitia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho aliyoyaagiza kufanyika katika sheria ya manunuzi kwa miradi yenye gharama ya kutoka shilingi bilioni 10 hadi shilingi bilioni 50 kupewa kipaumbele kutekelezwa na makandarasi wazawa ili kuwajengea uwezo.
Kuhusu madeni kwa Wakandarasi, Waziri Bashungwa amesema kuwa kupitia Wizara ya Fedha, Serikali imeshaweka utaratibu wa kulipa madeni hayo ambapo hivi sasa kila mwezi kuanzia mwezi Agosti 2023, kiasi cha shilingi bilioni 70 kinatengwa ambapo shilingi bilioni 50 zinalipa madeni ya Wakandarasi wa ndani na Bilioni 20 ni kwa ajili ya kulipa madeni ya Wakandarasi wa nje.
Waziri Bashungwa pia ameziagiza taasisi chini ya Wizara ya Ujenzi kuhakikisha zinabuni mikakati ya kutangaza mafanikio na kazi zao kwa umma ili kuleta tija katika Taasisi hizo na Taifa kwa ujumla. Hata hivyo, ameziagiza taasisi hizo kusimamia wataalam wao ili kuhakikisha wanatoa huduma sahihi na kwa wakati kwa umma na kuhakikisha wanachukua hatua kwa wale ambao watakiuka maadili ya kazi zao.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Mtendaji Mkuu wa NCC, Dkt. Matiko Mturi ameeleza kuwa kuwa Baraza hilo limefanikiwa kuandaa mapendekezo ya gharama za ujenzi wa barabara kwa kila mkoa wa Tanzania Bara na kuwasilisha katika kikao cha wadau wa ndani na kupata maoni na ushauri wao.
Vile vile, Msajili wa Bodi ya CRB, Eng. Rhoben Nkori, katika kuwasilisha taarifa yake amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, Bodi imesajili jumla ya miradi 4,374 yenye thamani ya shilingi Trilioni 9.274 ambapo miradi ya shilingi trilioni 4.999 sawa na asilimia 53.9 ilitekelezwa na Makandarasi wa ndani na miradi ya shilingi Trilioni 4.275 sawa na asilimia 46.1 litekelezwa na makandarasi wageni.
Naye, Msajili wa Bodi ya ERB, Eng. Benard Kavishe, amesema kuwa Bodi inaratibu mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi wahitimu yenye lengo la kuwawezesha wahitimu hao kupata ujuzi na umahiri wa kutosha katika utendaji wa shughuli za kihandisi katika muda mfupi.
“Katika kusimamia na kuratibu mpango huu wa mafunzo, Bodi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imeingiza katika mpango huu wahitimu 873 na kwa mwaka wa fedha 2022/23 wahitimu 2,113”, amefafanua Eng. Kavishe.
Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya AQRB, Arch. Edwin Nnunduma ameeleza kuwa Bodi imesajili jumla ya Wataalam 1,514 kati ya hao Wataalam Wazawa ni 1,481 na wageni ni 33. Kampuni za ushauri 455 kati ya hizo Kampuni za Wazawa ni 448 na za wageni 7. Kwa kipindi cha mwaka ujao wa fedha (2023/24) Bodi imepanga kusajili Wataalam 156 na Kampuni 30.
Waziri Bashungwa anaendelea na ziara ya kutembelea na kuzungumza na taasisi chini ya Wizara hiyo ili kujionea na kujadili mambo mbalimbali ya kuendeleza sekta ya ujenzi nchini.