JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UJENZI

BARAZA LA TAIFA LA UJENZI

Huduma Zetu

HUDUMA ZETU

Mafunzo

Mafunzo ni muhimu sana katika kukuza uwezo wa wadau wa sekta ya ujenzi. Mafunzo yanasaidia utendaji bora wa kazi ambao ni muhimu katika kukuza na kuongeza ubora na tija, pia kuwezesha kukabiliana na ushindani na kuleta thamani halisi kwa fedha zilizotumika katika miradi ya ujenzi.

Baraza linaendesha mafunzo kwa njia ya vitendo katika nyanja mbalimbali zinazohusiana na ujenzi zikijumuisha: ununuzi, usimamizi wa mikataba, usimamizi wa miradi, ukadiriaji wa gharama za ujenzi, sheria zinazohusiana na mikataba ya ujenzi,ukaguzi wa kiufundi, usuluhishi wa migogoro, menejimenti ya madai, mafunzo kwa makandarasi, ubia kati ya sekta binafsi na ya umma, ujenzi na matengenezo ya barabara kwa kutumia teknolojia ya nguvu kazi, matengenezo ya majengo pamoja na matumizi ya kompyuta katika ukadiriaji wa bei za majenzi na usimamizi wa miradi ya ujenzi.

Mafunzo pia yanatolewa kwa watu wenye mahitaji maalum kufuatana na mahitaji yatakayowasilishwa (Tailor made courses).

 Usuluhishi wa Migogoro

Tangu mwaka 1982 Baraza limeratibu migogoro katika sekta ya ujenzi kwa njia ya usuluhishi. Baraza limeandaa orodha ya Wasuluhishi wa migogoro katika sekta hiyo,wanaosajiliwa na kutumiwa na wadau kwa ajili ya usuluhishi wa migogoro inayojitokeza katika sekta. Aidha, utatuzi wa migogoro hufuata miongozo ya usuluhishi inayochapishwa na Baraza.

Ukaguzi wa Kiufundi

 Madhumuni ya kufanya ukaguzi wa kiufundi katika miradi ya ujenzi ni kuwasaidia wawekezaji/watoa fedha  kupata maelezo kuhusu mwenendo na utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na mapungufu yaliyopo, na utatuzi wake. Ukaguzi unaweza kufanyika katika hatua yoyote ya mradi ikiwa ni pamoja na matayarisho ya utekelezaji, wakati wa utekelezaji na baada ya mradi kutekelezwa. Baraza limekuwa likitoa huduma hii kwa serikali na taasisi zake na sekta binafsi, kwa mfano tangu mwaka 2005, Baraza limekuwa likikagua kupitia Wizara ya Fedha, miradi mikubwa inayogharamiwa na Serikali

Huduma za Ushauri

Baraza linashughulika na kutoa ushauri wa kiufundi katika mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya ujenzi; ikiwa ni pamoja na mipango kuhusu utekelezaji wa miradi, ununuzi na usimamizi wa mikataba ya ujenzi, usimamizi wa gharama za miradi, ukaguzi wa miradi kuhusu upatikanaji wa thamani ya fedha n’k.

Uratibu wa Sekta ya Ujenzi

Sera na Mikakati

 Baraza limehusika katika uratibu na uundaji wa sera na mikakati mbalimbali kwa ajili ya sekta ya   ujenzi kama ifuatavyo:

  • Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Ujenzi wa mwaka 1991
  • Sera ya Sekta ya Ujenzi ya mwaka 2003;
  • Mpango wa Utekelezaji wa Sera ya Sekta ya Ujenzi ya mwaka 2006.
  • Mwongozo wa ununuzi unaohusisha utekelezaji wa miradi kwa njia ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa mwaka 2008;
  • Rasimu ya Sera ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi ya mwaka 2008
  • Mapitio ya Sera ya Sekta ya Ujenzi ya mwaka 2017.

Vyama na Bodi za Usajili

Baraza lilihamasisha uundwaji wa bodi za usajili na vyama vya wadau wa Sekta ya Ujenzi ;ikiwa ni pamoja na:

  • Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB);
  • Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB);
  • Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB);
  • Chama cha Wabunifu Majengo (AAT);
  • Chama cha Wahandisi Washauri (ACET);
  • Chama cha Makandarasi wa Ujenzi (TACECA);
  • Chama cha Barabara (TARA).
  • Taasisi ya Usuluhishi na Migogoro (TIArb);
  • Taasisi ya Wakadiriaji Majenzi (TIQS);
  • Chama cha Wajenzi wa Sekta isiyo Rasmi (TAICO);
  • Mfuko wa Maendeleo wa Sekta ya Ujenzi (CIDF);

Makongamano ya Sekta ya Ujenzi

Kuanzia mwaka 2001, Baraza limekuwa likiandaa makongamano ya sekta ya ujenzi kila baada ya miaka miwili. Madhumuni ya makongamano ya Sekta ya Ujenzi ni kusaidia upangaji, uratibu pamoja na kuboresha maendeleo ya Sekta ya Ujenzi kwa kuzingatia yafuatayo:

  • Dira, malengo na mikakati ya maendeleo ya sekta ya ujenzi;
  • Mikakati ya kukuza uwezo ili kuboresha utendaji katika sekta;
  • Ukuaji wa sekta ili kukabiliana na ushindani wa Kimataifa;
  • Uhusiano wa kimataifa.

Utafiti

Kazi za utafiti zinazolenga katika kutambua matatizo mbalimbali na ufumbuzi wake yanayohusiana na sekta ya ujenzi kwa ujumla, ni mojawapo ya shughuli za Baraza. Tafiti zilizowahi kufanywa na Baraza ni pamoja na:

Tafiti kuhusu uanzishwaji wa mfuko maalum wa kuwasaidia wadau wa sekta ya ujenzi kupata mahali pa kukopa fedha au kupata dhamana kwa ajili ya miradi ya ujenzi;

  • Mahitaji ya mafunzo kwa washauri elekezi wazawa katika uhandisi wa barabara;
  • Mahitaji ya rasilimali watu katika sekta ya ujenzi nchini Tanzania;
  • Mahitaji ya mafunzo kwa washauri na wakandarasi wa miundombinu ya umwagiliaji katika kilimo;
  • Uanzishwaji wa mfuko endelevu wa mafunzo kwa wadau wa sekta ya ujenzi nchini;
  • Mapendekezo ya kuhuishwa sheria iliyoanzisha Baraza la Taifa la Ujenzi;
  • Utafiti kuhusu namna ya kuliwezesha kifedha, Baraza la Taifa la Ujenzi ili kuweza kutekeleza majukumu yake;
  • Utafiti kuhusu ajira katika miradi mikubwa nchini;
  • Mapitio ya kitaasisi na kisheria kutoka kuhusu ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi nchini;
  • Utafiti kuhusu wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi katika ujenzi.