Siku ya Wanawake Duniani: Wanawake NCC wasapoti maneno ya Samia

News Image Mar, 12 2021

WAKATI Dunia ikisherehekea Siku ya Wanawake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka waajiri wote nchini kutambua heshima ya mwanamke katika sehemu za kazi pamoja na kuwajali.

Aidha, amewataka kutambua changamoto za kibaiolojia zinazowakabili wanawake katika maeneo yao ya kazi, ili zinapotokea wasizitumie kama sababu ya kuwadharau, kuwanyanyasa au kuwanyima haki zao kwa namna yoyote.

Samia alisema hayo Mlimani City, Dar es Salaam wakati akihutubia mamia ya wanawake waliokusanyika mahali hapo kusherehekea kumbukizi ya Siku ya Wanawake Duniani.

Kwa mujibu wake, mwanamke ana tofauti ya kimaumbile ikilinganishwa na mwanaume hivyo, inawalazimu waajiri kulifahamu hilo na kuzijua changamoto anazozipitia wakati fulani anapokuwa katika wakati wake wa kuzipata changamoto hizo, wala si kutendewa yasiyofaa.

“Waajiri ambao ni mabosi hawana budi kuzifahamu changamoto za kibaiolojia wanazozipata wanawake walio katika maeneo yao ya kazi, lengo likiwa kuwasaidia na wala si kuwaumiza kwa kuwakomoa kufanya kazi zisizoendana na changamoto hizo kwa wakati husika”anasema.

Anaeleza kuwa haitakuwa sawa kwa mwajiri kutumia msemo wa 50 kwa 50 kumlazimisha au kumtuma mwanamke kufanya kazi fulani isiyoendana na hali yake wakati anapokuwa katika changamoto husika.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Bertha Mussa anasema Wanawake wa baraza hilo wanaunga mkono maneno ya Makamu wa Rais, Samia. Ameahidi kuhakikisha anakuza mahusiano mazuri ya kikazi kati ya wanawake na wanaume katika baraza hilo.

Mwenyekiti huyo pia amesema kwa faida ya NCC na taifa kwa ujumla, wanawake katika taasisi hiyo watahakikisha ushirikiano unadumishwa mahali pa kazi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha amani na upendo miongoni mwa wafanyakazi wote.

“Ili tufanye kazi kwa mafanikio ni lazima tufanye kazi kwa umoja na ushirikiano kama timu. Chamsingi cha kufanya ni kuhakikisha wanaume wanaeleweshwa kuhusu changamoto zetu za kibaiolojia ili zinapotupata wawe na ufahamu utakaowafanya wasitudharau au kutunyanyasa kwa kutupa kazi zisizoendana na changamoto hizo kwa wakati huo”.