​Majengo ya Serikali Kuwekewa Viwango Maalum

News Image Feb, 14 2024

Kwa muda mrefu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikijengamajengo yake kwa kutumia wataalam mbalimbali kutoka katika sekta ya ujenzi nchini. Wataalamu hawa wamekuwa wakitumia taaluma zao kuishauri serikali kulingana na kada zao kwa kutumia miongozo iliyopo. Miongozo ambayo imekuwa ikitumika ni ile inayotolewa na taasisi mbalimbali pamoja na viwango vilivyowekwa na nchi mbalimbali katika kuhakikisha kuwa majengo ya serikali yanafikia viwango vya ubora na usalama kulingana na mahitaji ya jengo husika. Miongozo hii imesaidia kwa kiasi fulani, japo bado imeshindwa kutumika katika maeneo yote yanayohitajia udhibiti wa ubora na usalama katika ujenzi wa majengo ya serikali pamoja na samani katika majengo ya serikali.

Hali hii imepelekea Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kuona umuhimu wa kuandaa Muongozo mmoja utakaotumika kudhibiti ubora na usalama katika maeneo yote ya ujenzi wa majengo ya Serikali pamoja na samani katika majengo ya Serikali. Katika kutekeleza jukumu hili, Wizara ya Ujenzi imekasimu kazi ya uandaaji Muongozo wa Viwango vya Ubora katika Ujenzi wa Majengo ya Serikali na Samani katika Majengo ya Serikali kwa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC). Kwa sasa NCC inaendelea kutekeleza jukumu hili kwa kuwashirikisha wataalam kutoka Idara na Taasisi mbalimbali za serikali zinazohusika na tasnia ya ujenzi.

Wataalam walioshiriki katika maandalizi ya Viwango hivyo ni wahandisi (umeme, mazingira, mitambo, TEHAMA, ujenzi), wasanifu majengo, wana usalama wamoto, majanga pamoja na wakadiriaji majenzi. Wataalam hawa wanatoka Wizara ya Ujenzi, Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, Wakala wa Huduma za Umeme, Mitambo na Elektroniki Tanzania (TEMESA) na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).

Ifahamike kuwa, tunapozungumzia viwango vya ubora katika ujenzi tunamaanisha muongozo au vigezo vya ubora wa kazi na vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa majengo ya serikali pamoja na samani katika majengo ya serikali. Viwango ambavyo vinaakisi viwango vya chini vya ubora vinavyohitajika katika ujenzi wa majengo ya serikali pamoja na samani katika majengo ya serikali. Viwango hivi vinawekwa ili kutoa sifa za kazi za ujenzi, vifaa na mitambo pamoja na kuhakikisha uthabiti, ubora, na usalama katika majengo na samani za Serikali.

UMUHIMU WA KUWEKA VIWANGO VYA MAJENGO YA SERIKALI

Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa NCC Mha. Heri Hatibu ambaye pia ndiyei kiongozi wa jopo la wataalamu linaloandaa rasmu ya Viwango vya Ujenzi wa Majengo ya Serikali pamoja na Samani katika Majengo ya Serikali, anaelezea umuhimu wa kuwa na nyaraka hiyo kwa kusema “Viwango vya Ujenzi wa Majengo ya Serikali pamoja na Samani katika Majengo ya Serikali ni muhimu kwa sababu kadha wa kadha” anazitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na:

Kwanza, kuleta usawa (msawazo/urari/ulinganifu) wa viwango katika majengo ya serikali, hii inamaanisha kuwa ujenzi wote wa majengo ya serikali pamoja na samani katika majengo ya serikali utazingatia viwango sawa vya ubora vilivyowekwa.

Pili, Kutawezesha kupunguza gharama za ujenzi, uendeshaji na matengenezo zinazotokana zaidi na ubora wa vifaa vya ujenzi vilivyoainishwa pamoja na mbinu zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi. Hili litawezesha kuboresha Uhai na kuimarisha usalama wa majengo ya serikali pamoja na samani katika majengo ya Serikali.

Tatu, Kuongeza uhakika wa usalama katika ujenzi wa majengo ya serikali pamoja na samani katika majengo ya serikali kwa kuwezezesha kustahimili changamoto mbalimbali, kama vile majanga ya asili, moto na ajali. Viwango hivi pia vitasaidia kulinda maisha ya watu na kupunguza hatari ya majeraha na vifo.

Nne, kwamba udhabiti wa majengo ni pamoja na kuhakikisha kuwa miundombinu inajengwa kwa nyenzo na mbinu zinazofaa. Hii itasaidia kuhakikisha uimara wa muda mrefu wa jengo na samani za serikali na hivyo kuzuia uwezekano wa kusababisha maafa.

Tano, kufikika kwa urahisi, katika kufafanua viwango vya ujenzi wa majengo ya serikali mara nyingi hujumuisha masharti ya ufikiaji, kuhakikisha kuwa majengo yanafikiwa na watu wenye ulemavu, huduma za kijamii na kutoa nafasi za udhibiti wa majanga yanapotokea.

Sita, Matumizi ya nishati mbadala: Viwango vya Ubora katika ujenzi wa majengo ya serikali pamoja na samani katika majengo ya serikali vimezingatia pia matumizi ya nishati mbadala kama vile matumizi wa umeme jua.

Saba, Viwango pia vimezingatia udhibiti wa uchafuzi wa mazingira kwa kuweka mifumo rafiki wa mazingira katika maeneo mbalimbali.

Mwisho, Manufaa ya kiuchumi, kuzingatia viwango vya ujenzi kunaweza kuwa na manufaa ya kiuchumi kwa kuvutia wawekezaji na biashara kwenye eneo hili, kuwezesha kuongezeka fursa za kazi katika ujenzi na viwanda vinavyohusiana, na kuongeza thamani ya mali.

Kwa ufupi, Mha. Hatibu anasisitiza kuwa, viwango vya ubora katika ujenzi wa majengo ya serikali pamoja na samani katika majengo ya serikali ni muhimu kwa kulinda maisha na mali, kukuza uendelevu na ufanisi wa nishati, kuhakikisha ufikivu na ushirikishwaji, na kukuza ukuaji wa uchumi na maendeleo.

Akiongelea sababu ya uandaaji rasimu ya miongozo hii kufanyika wakati huu alifafanua kuwa, moja ya majukumu ya Wizara ya Ujenzi ni kuhakikisha kazi za ujenzi zinazotekelezwa nchini ni salama, zenye ubora na zinazohakikisha kuwa thamani ya fedha inafikiwa ili kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi.

Ameongeza kuwa, katika kutekeleza jukumu hilo; Wizara kwa kushirikiana na taasisi zake pamoja na wadau wa tasnia ya ujenzi, imeendelea na uandaaji wa kanuni, miongozo na kuweka viwango vya kuzingatiwa katika shughuli za ujenzi.

Ifahamike pia kuwa, Muongozo huu utahakikisha kuwa kazi zote za ujenzi wa majengo ya Serikali pamoja na samani ambazo hazikuwa na miongozo huko nyuma, zimejumuishwa katika Muongozo huu.