Serikali ya Dk Samia kuendelea kuinua Wanawake-Waziri Mkuu
Mar, 11 2024WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kasim Majaliwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuinua wanawake nchini, katika nyanja zote .
Waziri Mkuu amesema hayo katika hotuba yake, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Hotuba hiyo imetolewa kwa niaba yake na mwakilishi wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima katika viwanja vya Shule ya Msingi Chinangali.
Katika hotuba hiyo, Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imefanya mambo mengi kwa ajili ya wanawake nchini na inaendelea kuhakikisha wanapata fursa na haki sawa.
"Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha kiuchumi wanawake 3,288,186 sawa na asilimia 54, kupitia mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Kwa mujibu wa Mhe. Majaliwa, Shilingi Bilioni 743.7 zimetolewa na kunufaisha Watanzania 6,064,957 wakiwemo wanawake hao, pamoja na wanaume 3,556,359 ambao ni asilimia 46.
Amesema, Serikali itaendelea kuinua wanawake kimitaji kwa kuwezesha upatikanaji wa mikopo nafuu, kwa sababu inatambua kuwekeza kwa mwanamke kwa kupitia mitaji ni kuinua uchumi wa jamii nzima.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu:"Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii.
Katika hatua nyingine, Wanawake wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), wameungana na wanawake wenzao kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali na za binafsi jijini Dodoma kuadhimisha siku yao wilayani Chamwino, Machi 08, mwaka huu.