Wafanyakazi NCC waungana na wengine kusherehekea Mei Mosi

KATIKA kutambua umuhimu wa Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) wameshiriki maandamano ya kumbukumbu ya siku hii pamoja na wafanyakazi wa mashirika, taasisi za Serikali, za binafsi na asasi za kiraia.
Maandamano haya katika mkoa wa Dar es Salaam yalianzia Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar-Es-Salaam (DUCE) na kuishia katika uwanja wa Uhuru uliopo wilayani Temeke jijini humo, ambapo ndipo shughuli zote za maadhimisho ya siku hii zimefanyika kimkoa.
Aidha, Wafanyakazi wa NCC wakiwa na bango lenye kubeba kauli mbiu ya Kitaifa isemayo Maslahi Bora, Mishahara Juu, Kazi iendelee, waliufikishia Umma ujumbe wa Baraza la Ujenzi kupitia bango hilo ikiwa ni njia moja wapo ya kuwahamasisha kujenga kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu.
Ujumbe wa baraza hilo unasema," jenga kwa kufuata ushauri wa kitaalamu kwaajili ya maendeleo yako na Taifa lako Tanzania".
Mfanyakazi hodari wa NCC
Sambamba na maadhimisho hayo, NCC imempata mfanyakazi wake Hodari kwa mwaka huu, QS Anitha Mallewo kutoka Idara ya Huduma za kiufundi aliyewashinda wafanyakazi wengine wanne kutoka idara nyingine tofauti. Alipata ushindi kupitia mfumo wa kura.Katika maadhimisho hayo, Mallewo alishiriki na kuifurahia siku yake kwa kucheza muziki kwa ustadi kulingana na midundo ya muziki iliyokuwa ikisikika wakati wa maandamano.