Wajumbe wa Bodi NCC, Menejimenti watembelea mradi mkubwa wa umeme Rufiji

News Image Feb, 02 2021

WAJUMBE wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) pamoja na menejimenti ya baraza hilo wametembelea mradi mkubwa wa kuzalisha umeme uliopo Rufiji mkoani Pwani na kujionea au kujifunza mambo mengi yaliyowathibitishia kuwa utakamilika kama ilivyopangwa katikati ya mwaka ujao.

Wajumbe hao wa bodi walioongozwa na Prof Mayunga Nkunya, na wanamenejimenti walioongozwa na Mtendaji Mkuu wa baraza hilo, Dk. Matiko mturi, walionyesha kufurahishwa kwao na maendeleo ya mradi huo ambapo walisema kwa nyakati tofauti kuwa unakwenda kwa kasi ya hali ya juu kiasi cha kwathibitishia kuwa huenda umeme mwingi wa kutoka katika bwawa la Julius Nyerere utapatikana mwakani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mradi huo walioutembelea hivi karibuni, Prof Nkunya na Dk Mturi wamesema umetokana na uthubutu wa Rais John pombe Magufuli kuruhusu mradi mkubwa na wagharama kama huo utekelezwe nchini, tena kwa fedha zetu wenyewe.

Meneja Usimamizi wa mradi huo kutoka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO),

Said Kambaya ndiye aliyewatembeza wajumbe na wana menejimenti hiyo katika miradi kadhaa midogo inayounda mradi huo mkubwa.

Anasema katika mradi wa umeme wa Julius Nyerere kuna miradi mingine midogo midogo kati ya tisa hadi 10.

Prof Nkunya kwa upande wake anasema Rais Magufuli amefanya uamuzi mgumu kuruhusu mradi huo na kwamba faida yake kubwa itaonekana baada ya muda fulani kupita, hivyo kuifanya Tanzania kuwa na maendeleo yanayokusudiwa.

Kwa mujibu wa Prof Nkunya. Wamefurahi kusikia kuwa licha ya ukweli kuwa mradi huo ni mgeni nchini, Watanzania kwa asilimia kubwa wameshiriki kwa utaalamu wao kuhakikisha unafanikiwa.

Vile vile, anasema, wamepata nafasi ya kujifunza mambo mengi waliokuwahawayajui.

Kwa maelezo ya Kambaya, asilimia 90 ya wataalamu wanaoshughulika kutekeleza mradi huo ni wa Tanzania na kwamba kampuni za nje zinazohusika pia kuutekeleza mradi huo kama wataalamu wakuu ni mbili tu za Urusi.

Aidha, amesema kampuni ya China imekuwa ikifanya usaidizi kwa kampuni hizo.

Kwa upande wake, Dk Matiko anasema mpango wa kutekeleza miradi mikubwa kama huo na wa reli ya SGR ilikuwepo tangu tulipopata uhuru lakini waliokuwepo walikuwa na woga wa kuruhusu miradi hiyo ianze kwa sababu ya gharama zake kuwa ni kubwa.

“Rais Magufuli ameweza na sasa tumefikia katika hatua nzuri itakayotuwezesha kuwa na umeme mwingi hata kuzidi mahitaji ya ndani ifikapo Juni 2022 . NCC tunampongeza”.alisea Dk mturi.,

Katika ziara hiyo, wajumbe wa bodi na wana menejimenti waliweza kujifunza mambo mbalimbali kupitia maswali waliyokuwa wakiyauliza ambayo, hata hivyo, yalijibiwa kwa ufasaha na Meneja wa mradi.