Dk Matiko: Watumishi wasipelekwe kozi ilimradi

News Image Nov, 30 2020

MTENDAJI Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Dk Matiko Samson Mturi, amewataka Wakuu wa Vitengo katika baraza hilo kuhakikisha wanaruhusu watumishi kushiriki mafunzo yenye tija kwao na taasisi, na wala si vinginevyo.

Amesema ni vyema mtumishi akapewa ruhusa kwenda kujifunza mambo yanayohusu eneo lake la kiutendaji (taaluma), ili ajiongezee ujuzi utakaomuwezesha kufanya kazi zake kwa ustadi wa hali ya juu na kuleta tija kwenye baraza.

Akizungumza katika kikao cha menejimenti ya Baraza hilo, Dk.Mturi ameitaka Idara ya Rasilimali Watu kuwa makini zaidi kuangalia vigezo muhimu vinavyotakiwa na baraza hilo katika masuala ya mafunzo yoyote, kabla ya kuruhusu mtumishi kuyashiriki.

Amesema maelekezo yake yanalengan kuboresha, kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kwa matumizi stahik, na si kunyima watumishi wa baraza haki yao ya msingi kupata mafunzo.

“Ni lazima tuzingatie mambo muhimu na kujiridhisha endapo mafunzo mtumishi anayokwenda kuyapata yanaweza kumsaidia katika kazi zake kwenye taasisi, kwa maana ya kumuongezea ujuzi, uelewa na maarifa anayohitaji katika kazi zake.

…kufanya hivyo kutatuwezesha kuepusha matumizi mabaya ya fedha za Serikali hasa tunazozitoa kama ‘perdiem’ na nauli. Tujitahidi ruhusa zisiwe ilimradi tu hata kama mtumishi kaalikwa kwa gharama za mualikaji, tuangalie kama mafunzo yanamchango wowote wa kitaaluma kwa mhusika na ikiwa yataweza kumfanya aisaidie taasisi kwa utaalamu anaokwenda kuupata,”amesema.

Aidha, amesema wakati umefika kwa kila mmoja kutunza muda wake wa kazi, kufanya kazi kwa weledi na kutumia ujuzi kwa ufasaha ili kuiletea NCC mafanikio.

“…Menejimenti na hasa wenzetu wa rasilimali watu msipeleke mtumishi kozi au kuruhusu aende kuhudhuria mafunzo kwa sababu kuna barua imeletwa ikimuita kuhudhuria mafunzo. Angalieni endapo kuna uhitaji wa mafunzo hayo na kama yanaweza kusababisha hatua fulani kwenye maendeleo ya baraza na ya mtumishi husika kitaaluma,” anaeleza.

Dk. Mturi amesisitiza kuwa kumpeleka mtumishi kozi ilimradi ni kumpotezea muda na hata kama mtumishi mwenyewe ndio anaomba kuhudhuria kozi isiyo na tija, wahusika katika rasilimali watu au viongozi wengine wa mtumishi huyo wanapaswa kumpa ushauri kuhusu kozi zinazomfaa kulingana na taaluma yake au uhitaji wa elimu hiyo.

Ameeleza kuwa ruhusa ya kuhudhuria kozi yoyote inayogharamiwa na NCC au taasisi nyingine nje ya baraza hilo isitolewe kwa yeyote ikithibitika kuwa kozi anayotaka kushiriki haina mchango kwa maendeleo ya mtumishi au taasisi.

“Kuruhusu mtumishi aende kwenye kozi za aina hiyo ni kumpotezea wakati na kutumia muda wa mwajiri kwa hasara…

Nasisitiza vigezo na masharti vitazamwe kwa umakini na kuzingatiwa ipasavyo, ili kila mtumishi apate nafasi kuhudhuria kozi zenye faida kwake na taasisi.

Menejimenti ya NCC imekaa katika kikao chake cha kawaida mwishoni mwa wiki.