‘Hatua ya awali ya uandaaji Sheria ya Majengo yakamilika’

News Image Dec, 21 2023

BARAZA la Taifa la Ujenzi (NCC) linaloratibu mchakato wa maandalizi ya Sheria ya Majengo nchini, limekamilisha hatua ya awali ya maandalizi ya sheria hiyo kwa kuandaa andiko dhana na kulikabidhi Wizara ya Ujenzi kwa hatua zaidi.

Mhandisi Ujenzi wa Baraza hilo, Geofrey Mwakasenga amesema Wizara ya Ujenzi imeipa NCC jukumu la kuratibu uandaaji wa sheria hiyo, ikiwa ni hatua moja wapo inayofanywa na Serikali kutatua changamoto zinazowakabili waendelezaji majengo nchini kwa kutokuwa na sheria hiyo.

Mhandisi Mwakasenga amesema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika uandaaji wa sheria hiyo, faida za kuwa na Sheria ya Majengo pamoja na changamoto zinazojitokeza wakati huu ambapo sheria hiyo haipo.

Kwa mujibu wake, maandalizi ya sheria ya majengo yanashirikisha wadau mbalimbali walio katika Sekta ya Ujenzi na nyingine, zikiwemo Wizara, taasisi mbalimbali za Serikali na za binafsi. Amesema andiko dhana hilo limebeba maoni ya wadau mbalimbali wa Sekta ya Ujenzi yanayoeleza changamoto zilizopo katika sekta ya ujenzi hasa katika eneo la ujenzi wa majengo. Pia, lime1jumuisha mapendekezo ya wadau hao kuhusu namna bora ya kutatua changamoto hizo ambayo kwa asilimia nyingi yameonesha kuwepo kwa uhitaji wa sheria hiyo ya majengo.

Usimamizi wa ujenzi wa majengo ulivyo sasa

Mhandisi Mwakasenga amesema kwa sasa usimamizi wa ujenzi wa majengo ni mgumu kutokana na ukweli kuwa sheria zinazousimamia ni nyingi na haziratibiwi na taasisi moja. Amesema hiyo ni changamoto kwa sababu inawapa usumbufu na kuwaongezea gharama zisizo za lazima waendelezaji majengo. “Sheria hizi, pamoja na uwingi wake, zinatoa mwongozo katika baadhi ya maeneo na kuyaacha mengine bila usimamizi,amesema".

Mhandisi Mwakasenga ametaja baadhi ya sheria zinazosimamia ujenzi wa majengo nchini kwa sasa kuwa ni pamoja na sheria za mipango miji, sheria ya afya na usalama mahali pa kazi, sheria ya zimamoto na uokoaji, sheria ya mazingira, sheria ya ukandarasi na usajili, pamoja na sheria zinazosimamia taaluma na wanataaluma katika fani za uhandisi, ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi.