Serikali Kuweka Miongozo ya Ujenzi Majengo Nchini

News Image May, 08 2023

Serikali inaandaa miongozo itakayotumika katika ujenzi wa majengo nchini ili kuhakikisha usalama, afya na ustawi kwa wanaotumia majengo hayo na jamii kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Mhandisi Dkt. Matiko Mturi wakati wa kikao kazi cha wataalamu wa sekta ya ujenzi wanaoshirikinkatika kuandaa rasimu ya viwango miongozo hiyo mjini Morogoro.

Dkt. Mturi ameeleza kuwa miongozoya ujenzi hiyo yaani Building Code vitatumika katika kusimamia ujenzi wa majengo yote yakiwemo ya Serikali, tasisisi binafsi na watu binafsi kwani utekelezaji utakuwa takwa la sheria ya kusimamia majengo nchini na kanuni zake. Amesema juhudi za kuandaa miongozo hii ilianza zaidi ya miaka ishirini iliyopita hivyo kwa sasa Serikali imedhamiria miongozo hii ikamilike na kuanza kutumika. Hivyo, viwango elekezi vinavyoandaliwa vitaondoa utata katika kujenga nyumba kwa matumizi mbalimbali, alisema Mkuu huyo.

Kwa muda mrefu ujenzi wa majengo nchini umekuwa ukisimamiwa kwa kiasi kikubwa na Sheria za Mipango Miji, Sura Na. 355 pamoja na kanuni za usalama wa moto katika majengo, sheria za Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na sheria nyingine. Aidha, viwango vya ubora wa majengo ulitegemea utashi wa mwenye jingo na wataalamu waliotumiwa kusanifu na kujenga majengo nchini. Hivyo, viwango elekezi vinavyoandaliwa vitaondoa utata katika kujenga nyumba kwa matumizi mbalimbali, alisema Mkuu huyo.

Kikao kazi cha kuandaa miongozo hii kinachoratibiwa na NCC kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kimekutanisha wataalamu wa sekta ya ujenzi wakiwamo wasanifu majengo, wakadiriaji majenzi, wadhibiti wa viwango, wadhibiti wa nishati, wahandisi umeme, wahandisi wa mifumo ya viyoyozi na maji, wataalamu wa vifaa vya ujenzi, wataalamu wa mazingira, zima moto na uokozi. Wataalamu hawa wametoka taasisi za Serikali na binafsi kwa nia ya kuweka pamoja maarifa, uzoefu, ustadi na weledi wao ili kuhakikisha miongozi hii inaandaliwa kwa ubora unaohitajika na kwamba ina uhalisia wa mahitaji ya kisekta na kutekelezeka vema.

Dkt. Mturi amesema kuwa baada ya kukamilisha mwongozo huu unaoeleza viwango katika ujenzi, taratibu za ujenzi zote zitaufuata na Serikali kupitia vyombo vyake itafanya ufuatiliaji na ukaguzi wa mara kwa mara ili lengo la kuwa na viwango bora na stahiki katika majengo vizingatiwe.

Mawanda ya miongozo hii yataenda kiasi cha kutambua kila hatua ya ujenzi wa majengo inapofika ikiwemo, viwango msawazo (specifications), usanifu wa jengo, maandalizi, ubora wa vifaa vya ujenzi vitakavyotumika kama vile matofali, nondo, saruji, misumari, mchanga pamoja na umahili na weledi wa wataalamu wanaojenga na kusimamia nyumba husika.

Akitoa maoni yake juu ya utengenezwaji wa viwango hivyo Mkadiriaji Majenzi na Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Thadeus Shio amesema “waraka huu umekuja muda muafaka kwani watu wanawekeza na kujenga majengo ya aina mbalimbali, akaongeza “lakini pia waraka huu utatoa uhakika kwa mtu anayewekeza maana anakuwa amefuata taratibu zote za ujenzi na hatokuwa amepingana na Sheria ya Ujenzi na Kanuni zake”.

Dkt. Shio amefafanua zaidi kuwa mabadiliko yanayotokea katika ubunifu na teknolojia hayana budi kuwa na waraka kama huu ambao utatoa mwongozo wa pamoja. Amesema utaratibu ukiwekwa na kusimamiwa na sheria hakutakuwa na utata katika shughuli za ujenzi maana kila anayeshiriki katika sekta hiyo atalazimika kuifuata. Hata hivyomtaalamu huyo alishauri Serikali kuhusika katika usimamizi wa waraka huukuanzia juu mpaka ngazi ya kijiji.

Aidha, mmoja wa washiriki katika kikao kazi hicho kutoka Jeshi la Zima Moto na Uokozi Mkaguzi Marwa Chacha alisema “mwongozo huu umekuja muda muafaka kwani utasaidia pia Jeshi la Zima Moto na Uokoaji katika utekelezaji wa majukumu yake” Aliongeza kuwa waraka utaweka uelewa wa pamoja kwa wadhibiti na wasimamizi wa majengo hasa upande wa usalama.

Kwa upande wake Mhandisi Brightson Njau kutoka Inter Consultant alieleza kuwa utakapoanza kutumia waraka huu, ujenzi holela utaondoka kutokana na kuongozwa nini cha kufanya na vifaa gani vitumike.

Mhandisi Njau akaongeza kuwa “Tanzania kuwa na mwongozo kama huu inaiweka nchi katika taswira nzuri ya kimataifa kwani wawekezaji wa nje ya nchi, wakifika Tanzania wanaulizia building Code zetu, hii huwafanya kutumia za kwao”.

Alisema baada ya kuwa na mwongozo huu, wawekezaji wa kimataifa katika ujenzi watakuwa na uhakika na maamuzi wanayoyafanya juu kuwekeza nchini Tanzania.

Vile vile, Mhandisi Dkt. Richard Mwaipungu kutoka Shirikisho la Wahandisi Washauri Tanzania anaipongeza Serikali kwa kuchukua hatua ya kuandaa building Code kwani kila mjenzi au mwekezaji, alikuwa anakuja na utaratibu wake lakini sasa tutakuwa na jambo zuri katika kuratibu shughuli za ujenzi nchini.

Mhandisi Mwaipungu anaona uwepo wa waraka huu na jinsi ulivyoweka viwango msawazo utasaidia katika kuangalia ubora wa viwango kulingana na vilivyoainishwa na matumizi yake. Anasisitiza kuwa “kwa kuwa waraka huu unaongelea viwango vya uuzaji wa vifaa vya ujenzi inafaa viuzwe na watu wenye ufahamu wa vifaa husika”.Akitoa mfano anasema “mtu akiuza vifaa vya umeme awe na taaluma ya umeme angalau ngazi ya cheti ili kuondoa ubabaishaji”

Kwa ujumla, mategemeo baada ya waraka hu kukamilika ni kuona ajira zinaongezeka kwani wataalamu mbalimbali katika ujenzi wa majengo watahitajika kutumika, kuwepo na utaratibu wa pamoja katika sekta ya ujenzi lakini tutarajie kuondoa vifaa na mifumo bandia kwani ni hatarishi kwa afya, usalama na ustawi wa watumisaji wa majengo nchini.

Kwa upande mwingine, nchi itakuwa na vigezo vyake mahsusi ambavyo vinaweza kutumika kimataifa pia. Katika mukhtadha huo huo, Tanzania itatambulika kimataifa kuwa na kanuni hizi.