​‘Usuluhishi nje ya Mahakama tiba ya mrundikano wa kesi’

News Image Apr, 27 2023

KWA kipindi kirefu mahakama nchini zimekuwa na changamoto ya mrundikano wa kesi mbalimbali, ambazo kwa namna moja au nyingine zingeweza kutafutiwa ufumbuzi nje ya mahakama, hivyo kuupunguzia mhimili huo mzigo usio wa lazima, pamoja na kusababisha upatikanaji wa haki kwa haraka.

Kutokana na hilo, Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limeona umuhimu wa kuendesha mafunzo kuhusu njia mbadala mbalimbali za kutatua migogoro ya kibiashara na ya madai ya kimikataba, nje ya mahakama. Migogoro hiyo ni ile inayohusisha sekta za biashara, ujenzi na nyingine.

Wakili Rusan Mbwambo amesema Dar es Salaam, wakati wa mafunzo kuhusu mbinu hizo mbadala za utatuzi wa migogoro ya kibiashara na madai ya kimkataba nje ya mahakama hivi karibuni kuwa, mbinu hizo, ikiwemo majadiliano (mazungumzo) hazichukui muda mrefu kuleta suluhu ya mgogoro husika.

Amesema ni njia bora kwa sababu zinawaacha wanaohusika na mgogoro kutoka katika pande zote, wakiwa na matokeo yasiyo jeruhi upande wowote kwa kuwa wahusika huhusika moja kwa moja kwenye usuluhishi kwa hatua zote, hivyo kuwa sababu kuu ya uamuzi wowote unaotolewa katika shauri husika.

Mbwambo amesema mbali na kutunza muda, mbinu hizo zimeonekana kuleta mafanikio kwa sehemu kubwa ykatika utatuzi wa migogoro mingi kutokana na ukweli kuwa, huwaacha wahusika wa pande zote mbili wakiwa na uhusiano mzuri unaoweza kuendelezwa kibiashara na hata kikazi, hasa kama unahusisha masuala ya kazi zinazo lazimu kuingiwa mikataba, hususan kwenye sekta ya ujenzi na nyinginezo.

“Unapotumia mbinu mbadala kutatua migogoro ya kibiashara na mingine nje ya mahakama unaokoa fedha ambazo zingetumika kulipia gharama mbalimbali za lazima kwenye mahakama ambako shauri linaendeshwa. Vile vile, wahusika wa pande zote mbili wanaweza kuamua ni nani ahusike kutatua mgogoro wao kati ya wanaopendekezwa, jambo linalowafanya wawe na imani na amani wakati wote mgogoro unapokuwa katika usuluhishi,”Wakili Mbwambo anasema.

Mbwambo ni miongoni mwa mawakili wabobezi katika masuala ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara na mingine ya madai ya kimkataba, nje ya mahakama na mahakamani pia. Ni mmoja ya wanaohusika kutoa mafunzo ya mbinu hizo kwa wadau wa Baraza la Taifa la Ujenzi ambapo, hivi karibuni, mafunzo hayo yameendeshwa kwa siku tatu mfululizo jijini Dar es Salaam. NCC ina jukumu la kutoa mafunzo mbalimbali ya kiwemo ya aina hiyo kwa wadau wake.

Kadhalika, Wakili Mbwambo anabainisha kuwa mahakama zina uwezo wa kisheria kuamuru shauri lolote la madai yawe ya kibiashara au yanayotoka kwenye sekta nyingine lirudishwe kwenye mfumo wa utatuzi migogoro wa awali, nje ya mahakama, hasa inapobainika na kuthibitika kuwa vipo vipengele vya mikataba vinavyo ainisha kuwa zitumike mbinu mbadala kutatua migogoro husika nje ya mahakama, kabla ya kuchukua uamuzi mwingine.

Anaeleza zaidi kuwa, miongoni mwa mambo ambayo wahusika kwenye mgogoro wa kibiashara, kimkataba pamoja na wakili anayefungua shauri mahakamani hawayataki nipamoja na kutumia muda mwingi kwenda mahakamani kusikiliza shauri na kusubiri uamuzi utolewe.

“Inapofikia wakati usuluhishi wa migogoro unahitajika, zipo njia mbalimbali za kuisuluhisha zinazoweza kutumika, ingawa huwawia vigumu wahusika wa pande zote mbili kufahamu ni ipi inafaa kuchaguliwa ili itumike kutafuta suluhu ya mgogoro uliopo kulingana na asili ya mgogoro wenyewe,”anasema.