Huduma za Ushauri wa kitaalamu.

Huduma za Ushauri wa kitaalamu.

27 May, 2026
Huduma za Ushauri wa kitaalamu.

HUDUMA ZA USHAURI WA KITAALAMU.

Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) hutoa huduma za ushauri wa kitaalamu katika maeneo mbalimbali yanayohusiana na utekelezaji wa miradi ya ujenzi na shughuli nyingine za sekta ya ujenzi.

Huduma hizi zinalenga kuwawezesha wateja kufanya maamuzi sahihi, kuboresha usimamizi wa miradi, kudhibiti vihatarishi, pamoja na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi, ubora na kupata thamani inayostahili.

NCC Hutoa Ushauri wa Aina Gani?

NCC hutoa ushauri wa kitaalamu katika maeneo mbalimbali ya sekta ya ujenzi, yakiwemo:

  1. Ushauri kuhusu uendeshaji na Usimamizi wa Miradi ya Ujenzi
    Ushauri kuhusu mipango ya utekelezaji, ufuatiliaji wa maendeleo ya mradi na utatuzi wa changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji.
  2. Ushauri kuhusu Usimamizi wa Mikataba ya Ujenzi
    Ushauri kuhusu tafsiri ya masharti ya mikataba, utekelezaji wa majukumu ya wahusika na usimamizi wa mabadiliko ya kimkataba.
  3. Ushauri kuhusu Mapitio na Tathmini ya Zabuni za Ujenzi
    Kufanya mapitio na tathmini ya zabuni ili kusaidia kuhakikisha mchakato wa uteuzi unazingatia mahitaji ya kiufundi, kifedha na thamani ya fedha.
  4. Ushauri kuhusu Mapitio ya Madai ya Wakandarasi (Contractor Claims Review)
    Tathmini ya uhalali wa madai, ushahidi unaowasilishwa na athari za madai hayo kwa utekelezaji wa mradi.
  5. Ushauri kuhusu Mapitio ya Mapendekezo ya Nyongeza za Mikataba (Addendum Reviews)
    Kutathmini sababu, uhalali na athari za mabadiliko yanayopendekezwa katika mikataba ya ujenzi.
  6. Tathmini ya Miradi ya Ujenzi
    Tathmini ya maendeleo ya mradi, ubora wa utekelezaji, utendaji na mafanikio ya malengo yaliyowekwa.
  7. Ushauri kuhusu Mabadiliko ya Bei za Ujenzi (Price Adjustments/Variations)
    Ushauri kuhusu mabadiliko ya bei za ujenzi na uhalisia wake katika gharama za mradi.
  8. Ushauri kuhusu Makadirio na Uchambuzi wa Gharama za Ujenzi
    Ushauri kuhusu tathmini ya gharama za ujenzi na udhibiti wa ongezeko la gharama za mradi.
  9. Ushauri katika masuala ya Migogoro ya Ujenzi (Construction Disputes)
    Ushauri na uchambuzi wa kitaalamu kuhusu migogoro ya ujenzi, pamoja na mapendekezo ya namna ya kutatua migogoro hiyo. NCC pia hutunza orodha ya Wasuluhishi (Adjudicators and Arbitrators) ambao wanaweza kutumika katika               michakato ya usuluhishi na utatuzi wa migogoro inapohitajika.

Nani Anaweza Kuomba Huduma za Ushauri?

Wadau wote wa sekta ya ujenzi wanaweza kuomba huduma za ushauri wa kitaalamu kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kulingana na mahitaji ya mradi au shughuli husika.

Jinsi ya Kuomba Huduma za Ushauri

Mteja anaweza kuwasilisha barua rasmi kwa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) akiomba huduma ya ushauri wa kiufundi.Endapo itahitajika, mteja anaweza kuomba NCC kuandaa Pendekezo la Kitaalamu (Proposal) kwa ajili ya utekelezaji wa huduma ya ushauri.Ili kuwezesha maandalizi ya pendekezo lenye ubora na linaloendana na mahitaji ya mteja, maombi yanashauriwa kuambatanishwa na Hadidu za Rejea (Terms of Reference – ToR) zinazoeleza kwa uwazi upeo, malengo na mahitaji ya kazi inayokusudiwa kufanyiwa ushauri.

Ada za Huduma za Ushauri wa Kitaalamu

Ada za huduma za ushauri hutegemea aina ya ushauri unaohitajika na mahitaji ya kazi husika.

Katika kuainisha ada, NCC huzingatia mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:

  • Aina na upeo wa ushauri unaohitajika;
  • Namna kazi itakavyotekelezwa;
  • Mbinu zitakazotumika katika utekelezaji wa kazi;
  • Eneo ambalo huduma ya ushauri itatolewa;
  • Ukubwa na kiwango cha ugumu wa kazi;
  • Muda unaohitajika kukamilisha kazi;
  • Idadi na utaalamu wa wataalamu watakaohusika; na
  • Rasilimali nyingine zitakazohitajika ili kuhakikisha huduma inatekelezwa kwa ufanisi na kutoa matokeo yanayotarajiwa.

Mteja Hupata Ushauri kwa Njia Gani?

Ushauri hutolewa kwa maandishi au kupitia mikutano, kulingana na mahitaji yaliyoainishwa katika Hadidu za Rejea (ToR) au makubaliano yaliyofikiwa kati ya NCC na mteja.

Je, Matokeo Hutolewa kwa Maandishi au Mikutano?

Matokeo ya ushauri yanaweza kutolewa kupitia:

  • Ripoti ya kitaalamu ya maandishi; au
  • Ripoti ya kitaalamu inayoambatana na uwasilishaji (presentation) kwa mteja na wadau husikaUwasilishaji wa matokeo unaweza kufanyika pale inapohitajika ili kueleza kwa kina hoja zilizobainika, uchambuzi uliofanyika na mapendekezo yaliyotolewa.

Kupitia huduma hii, NCC hutumia utaalamu wa kiufundi, uzoefu katika utekelezaji wa miradi na uelewa mpana wa sekta ya ujenzi kumsaidia mteja kuongeza ufanisi wa miradi, kupunguza vihatarishi na kuhakikisha uwekezaji unapata thamani iliyokusudiwa.