“Wanawake tumieni fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali”

WANAWAKE wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) wameungana na wanawake wengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Machi 08, kila mwaka ni siku ya Wanawake Duniani.
Mwaka huu, mkoani Dodoma, wanawake wa NCC wamejumuika na wenzao kutoka katika wizara, taasisi, mashirika, asasi za kiraia na jumuiya mbalimbali za kitaifa na kimataifa zilizopo mkoani humo kuiadhimisha siku hiyo kwa kushiriki maandamano wilayani Kondoa, ilipoadhimishwa kwa ngazi ya mkoa.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule.
Kitaifa, maadhimisho hayo yamemebwa na Kauli mbiu isemayo “Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia katika Kuleta Usawa wa Kijinsia,” huku NCC nayo ikiwa na kauli mbiu yake isemayo “Wanawake ni nguzo muhimu katika Sekta ya Ujenzi”.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Bi. Senyamule amewashauri wanawake wachangamkie fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali, ikiwa ni pamoja na kuunda vikundi ili iwe rahisi kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha, kwa ajili ya mitaji ya biashara itakayosaidia kuinua uchumi wao.
Pia, amewataka wajiendeleze kwa kutumia program zinazotolewa na taasisi wezeshi za Serikali kama vile Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), zinazosaidia wajasiriamali nchini katika masuala mbalimbali ya kukuza uwezo wao kwenye uzalishaji, ikiwemo matumizi ya teknolojia na uzingatiaji viwango vya ubora.
Mkuu wa Mkoa amewataka wanawake na wananchi kwa ujumla kutambua jitihada za Serikali katika kulinda haki za wanawake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha sheria inayoelekeza uwezeshaji wa mikopo nafuu kwa wanawake inazingatiwa.
“Mbali na hayo, leo tunazindua Wanawake na Samia mkoani Dodoma, ili mama Samia anapotekeleza miradi mikubwa, wanawake viongozi wa mkoa wa Dodoma wanaiounda kamati hiyo wamsaidie kutatua changamoto mbalimbali katika mkoa huu kwa nafasi zao,”amesema”.