NCC yashiriki Bonanza la Michezo la Wizara ya Ujenzi

BARAZA la Taifa la Ujenzi (NCC), limeshiriki Bonanza la Michezo kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma na baadhi ya watumishi wake kuibuka kidedea katika mashindano ya michezo mbalimbali iliyoandaliwa, ikiwemo riadha, karata, bao, mpira wa miguu na kukimbiza kuku.
Bonanza hilo limefanyika Jumamosi kuanzia saa 12:00 asubuhi, ambapo washiriki kutoka Wizara ya Ujenzi na taasisi zake walianza mbio za kupasha mwili joto (Jogging) kutoka katika eneo la nje ya Bunge hadi kwenye Uwanja wa Jamhuri, ambapo mashindano yalifanyika.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ujenzi iliyoandaa bonanza hilo, ni maalum kwa ajili ya afya za watumishi, uhusiano unaohusisha kufahamiana pamoja na kufurahi.
NCC iliwakilishwa na washiriki 20 waliogawanyika katika makundi tofauti kulingana na michezo waliyoshiriki; palikuwa na kundi la wavuta kamba, wanariadha, wakimbiza kuku, wacheza mpira wa miguu na netiboli.
Aidha, katika mpira wa miguu uliohusisha timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) pamoja na wapinzani wao ambao ni timu iliyojumuisha watumishi kutoka katika taasisi zake miongoni mwazo ni NCC, Ramadhani Mwaikandage kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi alikuwa wa kwanza kupachika bao katika wavu wa goli la wizara, ingawa wizara nayo ilipata bao moja baadaye kwa njia ya penati lililosababisha matokeo ya goli 1 kwa 1.
Katika riadha, Bi. Sada Nassoro wa NCC alishika nafasi ya kwanza kwa kumaliza vizuri mbio za Mita 100 na kuwashinda wengine.
Vile vile, Katika mbio za kukimbiza kuku aliyeachiwa kwenye eneo la wazi la uwanja huo, Changwe Kitmer wa NCC aliyeshinda katika mchezo wa karata, alifanikiwa kumkamata kuku aliyekuwa akishindaniwa na kujitwalia kitoweo kutokana na juhudi zake.
Kipengele hiki cha kukimbiza kuku kilikuwa na raha yake hasa baada ya kuamuliwa washiriki wa mchezo huo waurudie kutokana na kilichoelezwa kuwa Bw. Kitmer alimkamata kirahisi.
Hata hivyo, pamoja na kurudiwa, ushindi uliendelea kuwa wa Bw. Kitmer kutokana na ukweli kwamba alifanikiwa kumdaka kuku kama alivyofanya awali, hivyo meza kuu kumtangaza kuwa ndiye mshindi.
Bw Kitmer aliruhusiwa kuondoka na kuku huyo kwa ajili ya matumizi aliyoona yanafaa iwe kitoweo au mengine yaliyokuwa ndani ya uwezo wake. “Kuku huyu nimempata wakati muafaka, ninakwenda kumchinja na kumgeuza kitoweo”, anasema Bw. Kitmer.