​NCC yakutanisha wadau wa Sekta ya Ujenzi nchini kusikia maoni yao

News Image Dec, 16 2021

NCC yakutanisha wadau wa Sekta ya Ujenzi nchini kusikia maoni yao

  • Ni kuhusu maendeleo ya Sekta ya Ujenzi Tanzania
  • Kupata mawazo yao na mapendekezo kuhusu kanuni za Sheria ya NCC

BARAZA la Taifa la Ujenzi (NCC) limefanikiwa kuwakutanisha wadau wa Sekta ya Ujenzi nchini kwa lengo la kupata maoni yao kuhusu maendeleo ya sekta ya ujenzi Tanzania, pamoja na kusikia maoni na mapendekezo yao kuhusu masuala mbalimbali ya sekta hiyo yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kuikuza zaidi kwa maendeleo ya taifa.

Mkutano huo unafanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam kwa siku mbili; Disemba 15 na 16 ukiwa na mada kuu mbili; inayozungumzia maendeleo ya Sekta ya Ujenzi nchini kwa kuangazia tulipotoka kama nchi katika eneo hilo la sekta ya ujenzi, tulipo, tunapoelekea na kusikia mawazo ya wadau kuona nini kifanyike kuhakikisha sekta hiyo inapanuka zaidi au inakua zaidi kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Katika mkutano unaoendelea leo, wadau wanajadili mada ya pili inayohusisha kanuni za sheria ya NCC zilizo katika mchakato wa kuanzishwa, ili kuona ni zipi zinafaa na zibebe nini ndani yake kwa lengo pia la kuhakikisha baraza hilo linaendeshwa kwa namna itakayoisaidia zaidi Sekta ya Ujenzi na nchi kwa ujumla kufikia malengo yake hasa kwa upande huo wa eneo la ujenzi.

Mkutano huo umefunguliwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Prof Riziki Shemdoe aliyelipongeza Baraza la Taifa la Ujenzi kwa kufanya maboresho mbalimbali ya kisekta yanayochangia kuikuza sekta ya ujenzi nchini ambayo ni pamoja na kuendesha mafunzo kwa wadau wa sekta hiyo yanayowajengea uwezo wa kiutendaji, kuhakikisha uanzishwaji wa bodi za usajili wa kisekta na kuratibu utatuzi wa migogoro mbalimbali katika sekta ya ujenzi nchini.

Amesema,”Tunalishukuru Baraza la Taifa la Ujenzi kwa kufanikisha mambo hayo na tuna kiu kubwa ya kusikia wadau wa sekta ya ujenzi hususan wasimamizi wa sekta hii ya ujenzi mnajadili nini katika mkutano huu muhimu.”

Amewataka wadau wote wanaopata nafasi ya kutoa mawazo na maoni kuhusu kanuni za sheria ya NCC zilizokatika mchakato wa kuanzishwa, wafanye hivyo huku wakifahamu kuwa zinaanzishwa kwa madhumuni ya kusaidia watu wote na sekta nzima ya ujenzi inayowahusiaha wakiwemo wao, wala si kwa ajili ya mshauri elekezi pekee.

Kulingana na hilo, Prof Shemdoe amewashauri wadau wote wanaoshiriki mkutano huo kutosita kueleza yote wanayoona kuwa ni muhimu na yenye kuweza kusaidia kutengenezwa kwa kanuni bora za sheria hiyo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa NCC, Dk Matiko Mturi amesema mafanikio ya Sekta ya Ujenzi yanawategemea wadau wote wa sekta hiyo hivyo hawana budi kutoa ushirikiano wa dhati kwenye mambo yote muhimu wanayoshirikishwa wakati wote yanapohitajika.

Aidha, mtoa mada kuu katika siku ya kwanza, Mhandisi Prof Awadhi Mawenya amesema, ikiangaliwa mahali sekta ya ujenzi ilipotoka na ilipo sasa inaonesha kuwepo kwa matumaini ya kufanya vizuri zaidi kisekta katika siku zijazo ikiwa maeneo yote yanayoonekana kuhitaji maboresho yataboreshwa.

“Ikiwa tutajipanga vizuri zaidi na kufanya maboresho yote yanayotakiwa katika sekta ya Ujenzi nchini tutaweza kuifikisha mbali kimaendeleo kwa sababu uelekeo wake kwa siku zijazo unaonekana kuwa wenye mwangaza au nuru,”amesema.