NCC yaitumia Wiki ya Utumishi wa Umma kutembelea miradi • Yatoa ushauri wa kitaalamu kuhusu ujenzi

News Image Jun, 23 2022

BARAZA la Taifa la Ujenzi (NCC) kwa kutumia wataalamu wake wa masuala ya ujenzi, limetembelea miradi mitatu ya ujenzi wa ofisi za Serikali, inayotekelezwa na Vikosi vya Ujenzi vilivyo chini ya Sekta ya Ujenzi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala mbalimbali ya ujenzi kwa watekelezaji wa miradi hiyo.

Ziara hiyo imefanyika wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma inayofikia kilele leo.

Miradi iliyotembelewa inatekelezwa katika Mji wa Serikali Mtumba uliopo jijini Dodoma. Kwa mujibu wa wasimamizi wa miradi hiyo, kila mmoja unapaswa kukamilishwa ndani ya kipindi cha miaka miwili tangu ulipoanza, kulingana na matakwa ya mkataba wa mradi husika. Kwa maelezo yaliyotolewa kwa NCC, imeanza kati ya Oktoba 2021 na Januari 2022.

Timu ya wataalamu hao kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi imeongozwa na Mhandisi Moses Lawrence, ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Kiufundi.

Katika miradi mitatu iliyotembelewa, miwili inasimamiwa na wanawake kwa cheo cha Meneja Mradi ambayo ni ; ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, unaosimamiwa na Mhandisi Ensi Japhet na mradi wa ujenzi wa ofisi za TAMISEMI unaosimamiwa na Mhandisi Suma Atupele. Hata hivyo, ujenzi wa ofisi za Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, katika eneo la ujenzi wenyewe (site)unasimamiwa na Mhandisi Neema Siwako kwa nafasi ya Meneja wa ‘saiti’ (Site Manager).

Wakati wa mazungumzo na wasimamizi wa miradi hiyo waliohusisha wahandisi, wasanifu majengo na wakadiriaji majenzi ambao wataalamu wa NCC wamekutana na kukaa nao kwa nyakati tofauti kwenye maeneo yao ya miradi,

Ilipatikana fursa kwa wahusika wanaotekeleza miradi hiyo kutoka Vikosi vya Ujenzi kuuliza maswali, kutoa maoni kuhusu maeneo mbalimbali yanayohusu ujenzi pamoja na kupokea ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa baraza hilo.

Aidha, wameeleza masuala mbalimbali likiwemo la mfumuko wa bei za bidhaa za ujenzi kuwa changamoto kubwa katika utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo, ingawa wamesema kwa nyakati tofauti kuwa kazi ya ujenzi ni lazima iendelee.

Wasimamizi wa miradi yote wameigusia changamoto hiyo kwa nyakati tofauti na kueleza kuwa si tu kwamba inatishia ‘kutingishika’ kwa faida wanayotegemea kuipata, bali inakatisha tamaa.

“Kazi lazima iendelee. Mfumuko wa bei unatuathiri lakini si kwa kiasi chakusema kuwa hatutafanya kazi”, anasema Mhandisi Bi. Japhet anayesimamia mradi wa ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Meneja Msaidizi wa mradi wa ujenzi wa ofisi za TAMISEMI, Mhandisi Valence Ngashweki ameiomba NCC iishauri Serikali ifanye jambo kuhakikisha mfumuko huo wa bei hauwaathiri kwa kiasi kikubwa kwa sababu kazi ya Serikali ni lazima iendelee na ikamilike. “Serikali inaweza kufanya jambo…Ninaomba NCC iishauri ilifanye jambo hilo ili tupate unafuu, kwa sababu bei za bidhaa za ujenzi inazidi kupanda na kutuathiri”.

Naye Mhandisi Ally Lusesa anayesimamia mradi wa ujenzi wa ofisi za Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anasema hali ya kupanda kwa bei ‘inawatingisha’ kwa kiasi kikubwa hivyo ni vyema ikadhibitiwa kwa namna Serikali itakayoona kuwa inafaa.

Sambamba na hayo, wataalamu wa NCC waliwasisitiza kutumia vifaa vya usalama kazini kama vile glavu za mikono na viatu vigumu (boots) ili kuzuia madhara makubwa endapo wataumia kwa bahati mbaya wakiwa kazini.

Mbali na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu ujenzi, NCC imepata nafasi kueleza kuhusu mafunzo inayotoa kwa wadau wa ujenzi pamoja na shughuli nyingine inazozifanya.

Akimalizia, Mhandisi Lawrence kutoka NCC amejibu, “Tuliowashauri yafanyieni kazi, lakini hhata hivyo tunapenda mfahamu kuwa tumewasikia, maoni yenu tumeyasikia na tunakwenda kufanyia kazi kama mlivyoomba”.