NCC yamtakia Njaila mafanikio mema baada ya kustaafu

News Image Jul, 01 2021

BODI ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) inamtakia mfanyakazi aliyestaafu Utumishi wa Umma hivi karibuni, Eliud Njaila mafanikio na maisha mema popote atakapokuwa baada ya utumishi wake serikalini.

Njaila aliyeanza Utumishi wa Umma katika Wizara ya Afya mwaka 1990 amestaafu siku chache zilizopita katika Baraza la Taifa la Ujenzi akiwa Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi (PMU). Alizaliwa tarehe 18, Disemba mwaka 1965.

Njaila anayetajwa karibu na wafanyakazi wote wa NCC kuwa ni kiongozi, kaka na rafiki mcheshi, mnyenyekevu na mwenye busara aliamua kustaafu kwa hiyari akiwa na sababu zake za msingi.

Kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mtumishi wa Umma anaruhusiwa kustaafu kwa hiyari akiwa na umri wa miaka 55. Hata hivyo, sheria inasema Mtumishi wa Umma anapaswa kustaafu kwa mujibu wa sheria anapofikisha umri wa miaka 60.

Wakati wa hafla fupi ya kumuaga Njaila iliyofanyika jana mchana katika ukumbi wa NCC uliopo kwenye Mtaa wa Mansfield, Dar es Salaam, alitaja ofisi kadhaa za Serikali alizowahi kufanya kazi pamoja na kueleza uzoefu wake katika Utumishi wa Umma.

Maelezo kuhusu uzoefu wake huo yaliwafanya wafanyakazi wa NCC kuamini kuwa Njaila ni Mwalimu mzoefu anayeweza kufuatwa kwa ushauri wakati wowote atakapo ruhusu na kutoa funzo fulani kuhusu Utumishi wa Umma kwa atakaye hitaji.

Akitoa neno la shukrani, Njaila alieleza siri ya kufanikiwa kwake kufanya kazi kwa kipindi hicho chote Serikalini kuwa ni bidii ya kazi.

“Nina wausia fanyeni kazi kwa bidii. Lakini pia waajiri pamoja na menejimenti hakikisheni mnawapa wafanyakazi vifaa vya kazi vinavyohitajika kwa wakati na kuwaandalia mazingira mazuri na bora ya kazi ili nao waweze kutimiza wajibu wanaopewa kama inavyopasa,” Njaila alisema.

Njaila amejifunza nini NCC?

Njaila alisema alipojiunga NCC siku za kwanza aliona kuwa ni taasisi inayoweza kuwa kubwa zaidi na hata kurejea katika uelekeo wake wa mwanzo uliokusudiwa ikiwa itakuwa na kanuni zitakazoiwezesha sheria ya taasisi hiyo kufanya kazi kwa ufasaha. Alisisitiza kuwa mchakato wa kutengeneza kanuni hizo uendelezwe na kufikia mwisho wenye mafanikio, ili kanuni zianze kutumika.

Kwa mujibu wake, aliona pia kuwa NCC inaweza kuwa na mchangamano mkubwa na taasisi nyingine hivyo kufikia lengo la kuanzishwa kwake na ikibidi zaidi ya hilo.

Neno kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu

Dk. Matiko Mturi ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa NCC, alimtaja Njaila kuwa shujaa kutokana na uamuzi mgumu aliouchukua wa kustaafu kabla ya muda wa kustaafu kisheria.

Dk. Matiko alisema huo ni ujasiri wa hali ya juu kwa sababu watumishi wengi wa Umma huhofia kustaafu na hasa wanapokaribia umri wa kufanya hivyo wengi huwa na mashaka.

“Kwa Njaila ilikuwa tofauti, alipotuambia kuwa anataka kustaafu kwa hiyari nilisema moyoni huyu mtu ni jasiri, lakini nilipojua kuwa ni uamuzi ambao alikuwa ameufanya pia baada ya mashauriano na wanafamilia yake nikasema ni jambo la heri linaloonyesha uthubutu ambao wengine tunapaswa kuuiga,”alisema Dk Matiko.

TAMICO nayo haikubaki nyuma

CHAMA cha Wafanyakazi TAMICO-Tawi la NCC nacho kupitia mwakilishi wa viongozi wake, Tumaini Masige kilitoa pongezi kwa Njaila na kumtakia heri na mafanikio katika mambo yote atakayokwenda kuyafanya baada ya kustafu kwake popote atakapokuwa.

Kupitia mwakilishi huyo, Chama hicho pia kilimwita Njaila kuwa ni shujaa kutokana na uamuzi aliouchukua. Aidha, kiliwashauri wengine kuiga mfano huo.

Njaila, pamoja na mambo mengine, alikabidhiwa cheti.