Mwakibete aiambia Bodi ya NCC: Mkiwa na shida semeni

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amewataka wajumbe wa Bodi ya NCC aliyoizindua kutojiona yatima wakati wa kufanya kazi zao pindi wanapokumbana na changamoto zinazohitaji msaada kutoka wizarani.
Naibu Waziri Mwakibete amewaambia wajumbe hao kuwa wana haki ya kuomba msaada wakati wowote wanapouhitaji ili wasikwame kutekeleza wajibu wao wa kuisimamia NCC ili nayo iweze kufanikisha shughuli zake za msingi, kama inavyotakiwa kisheria.
Amesema, “Wizara yenu (Ujenzi) ipo tayari kuwasaidia hiyo msisite kuikaribia mnapopata changamoto wakati wa utekelezaji wa majukumu yanu ya bodi na wala msijione kuwa ni yatima…Sisi tupo na tuko tayari kuwasaidia,”.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mwakibete, pamoja na kuwapa wajumbe hao wa bodi maelekezo ya kuweka alama kwa kusababisha maendeleo katika NCC ndani ya miaka mitatu ya kipindi chao cha kazi katika bodi hiyo, amewaasa wasifumbie macho vitendo vyovyote vinavyoweza kulizorotesha Baraza la Taifa la Ujenzi wala wasikubali rushwa ya aina yoyote kutoka kwa mtu yeyote anayeweza kupita kwenye ‘mstari’ wao.
Kadhalika ameitaka bodi hiyo si tu iisaidie NCC kuweza kutekeleza majukumu yake, bali iifanye sekta ya ujenzi na tasnia zilizo ndani ya sekta hiyo ziheshimike.
Mwenyekiti wa Bodi ya NCC aahidi mambo mazuri
MWENYEKITI wa Bodi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Dk Fatuma Mohamed ameahidi kwa niaba ya wajumbe wote wa bodi hiyo kutekeleza wajibu unaowapasa kwa juhudi na maarifa,ili kuhakikisha NCC inafanikisha kazi zake kwa ufanisi, hivyo kuleta tija kwa taifa, kupitia sekta ya ujenzi.
Amesema hayo baada ya bodi hiyo kuzinduliwa na kukabidhiwa vitendea kazi, ikiwemo Sheria ya NCC.
“Tarajieni kuona tukitekeleza majukumu mliyotupa ipasavyo.” Dk. Fatma anasema wanaelewa umuhimu wa Baraza la Taifa la Ujenzi katika nchi na kwa sekta ya ujenzi, hivyo wako tayari kutumia weledi na ujuzi wao kuhakikisha wanasimamia maeneo yote wanayopaswa kuyasimamia kuhakikisha yanafanya vizuri.
Ilielezwa katika uzinduzi huo kuwa asilimia 14 ya mchango wote katika pato la taifa inatoka kwenye Sekta ya Ujenzi, hivyo wana kila sababu ya kuhakikisha kuwa inaendelea mbele.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi), Ludovick Nduhiye amewaambia wajumbe wa Bodi mpya ya NCC kuwa uteuzi wao umetokana na kuaminiwa kwao si kwa maneno tu bali kwa kuzingatia uwezo wao katika kazi.
Amesema, “kutokana na weledi na ujuzi wenu, tambueni kuwa mna kazi kubwa ya kuwaendeleza wakandarasi wa ndani, pamoja na taaluma mbalimbali zilizo katika sekta ya ujenzi, Sisi kama wizara tutawapa ushirikiano wa kutosha pale mtakapouhitaji ili lengo letu la kuifanikisha sekta hii ya ujenzi lifanikiwe”.