Mei Mosi Dodoma yafana, Mtendaji Mkuu NCC ashiriki

News Image May, 04 2023

MTENDAJI Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Dk Matiko Mturi, ameungana na watumishi wa Baraza hilo, pamoja na wafanyakazi wengine duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Kitaifa maadhimisho hayo yamefanyika mkoani Morogoro, mgeni rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk. Samia Suluhu Hassan. Dodoma, maadhimisho hayo ambayo Dk Mturi ameshiriki yameanza kwa maandamano yaliyojumuisha vyama mbalimbali vya wafanyakazi, kuanzia viwanja vya Bunge hadi uwanja wa Jamhuri, huku yakiwa yamebeba kauli mbinu ya mwaka huu 2023 isemayo: “Mishahara bora na ajira zenye staha ni nguzo kwa maendeleo ya wafanyakazi,wakati ni sasa!”

Taasisi na mashirika mbalimbali ya Umma, ya Serikali na binafsi, ya kitaifa na kimataifa, wizara pamoja na waalikwa wengine wakiwemo majirani, wafanyabiashara kubwa na ndogo nao wameshiriki maadhimisho hayo.

Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Mhe. Jumanne Sagini ametoa ujumbe kuwaasa wafanyakazi ambao ni wazazi na au walezi kutosahau jukumu jingine la malezi bora ya watoto wakati wakitekeleza majukumu yao ya kila siku kazini.

Kwa mujibu wa Mh Sagini, jukumu la kulea watoto katika misingi ya maadili ni la msingi kwa kila mtu,hasa wazazi,hivyo kuwa waajiriwa au waajiri katika kazi fulani hakupaswi kuwa sababu ya kuacha jukumu hilo.

Mbali na hayo,Naibu Waziri Sagini ametoa wito kwa waajiri nchini kutowachagulia wafanyakazi wanao waongoza vyama vya wafanyakazi wanavyovitaka wao, kwa sababu zao kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa.

Amesema, wafanyakazi katika eneo fulani la kazi iwe taasisi, shirika, kampuni au wizara wana haki ya kuamua chama cha wafanyakazi cha kujiunga nacho, hivyo wasisitizwe kujiunga lakini wasichaguliwe chama kwa mtazamo wa mwajiri.

Anasema lengo ni kuwafanya wawe huru kutoa yao ya moyoni, kuchangia maoni na kusababisha mambo yaende sawa katika mahali pao pa kazi.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa TUCTA Dk Leonia msafiri amemshukuru Dk Samia kwa niaba ya wafanyakazi nchini kwa kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi siku hadi siku.