Katibu Mkuu Ujenzi: Lindeni taswira ya NCC

News Image Dec, 21 2020

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, anayeshughulikia sekta ya Ujenzi, Elius Mwakalinga amewataka wafanyakazi wa Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC) walinde taswira ya taasisi hiyo kwa kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo na maadili, bila kufikiria kwanza ‘chochote kitu’ kinachoweza kutolewa kama motisha.

Aidha, amesema hana utartibu wa kumchukulia mtumishi yeyote mwenye tabia ya uharibifu ambaye hata akionywa mara mbili hurudia makosa yale yale.

Amesema hayo wakati wa kikao cha Tatu cha Baraza la Wafanyakazi wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) kilichofanyika Dar es Salaam hivi karibuni.

Amesema kwake makosa kama wizi na uharibifu mwingine unaoiletea taasisi au sekta taswira mbaya ni sababu tosha ya kumfukuza kazi muhusika, ilimradi tu awe amemuonya mara ya kwanza na ya pili.

“Kwangu mimi motisha ni tofauti, ukiharibu motisha ninayokupa ni adhabu. Ukifanya uharibifu kwa mfano nisikie kuwa umeiba, mimi nitakuita mara moja halafu ukirudia nitakuita mara ya pili kukuonya, lakini ukirudia nakufukuza hapo hapo na wakati huo huo”, Mwakalinga amesema.

Ameweka wazi kuwa katika utendaji wake, hamchukuliikuwa bora mtendaji anayependa kujibidisha kwa sababu tu yakujua kuwa kuna chochote kitu cha ziada anaweza kupewa na uongozi wa taasisi pindi akionekana kuwa anafanya kazi kwa bidii.

Amesema anachoangalia ni endapo mtumishi huyo anaweza kujituma bila kusimamiwa au bila kuchochewa kufanya hivyo na motisha.

“Mtumishi bora ni yule anayejituma wakati wote kwa kuipenda kazi yake, hata kama haina motisha au malipo ya ziada, ni yule anayezingatia matakwa yote muhimu ya kiutendaji na uwajibikaji katika kazi pamoja na kuijali kazi husika.

Kwa maelezo yake, uwezo wa kazi ni lazima uendane na kuijali kazi husika,si kuwahi ofisini tu na kuzunguka kusalimia kila mtu katika kila ofisi hadi saa zinaishia katika kusalimiana.

Amefafanua kuwa uwezo wa kazi ni pamoja na kuilinda, kuipenda, kuithamini na kujitoa kwayo kwa moyo, bila kujali mengineyo.

Amesema mtu anayefanya kazi vizuri kwa sababu ya kutaka aonwe na kupewa chochote cha ziada anakuwa ni mwenye kusukumwa na ‘kitu’ wala si utu wa kazi.“Mtu wa aina hiyo akikosa chochote kitu hawezi kufanya kazi kama inavyotakiwa,”amesema.

Kuhusu kulinda taswira ya taasisi, Katibu Mkuu amesema ni jambo linalompasa kila mfanyakazi, aliye na cheo na hata asiye na cheo.