Katibu Mkuu TAMISEMI akumbusha wakandarasi wa barabara jambo jema
Katibu Mkuu TAMISEMI akumbusha wakandarasi wa barabara jambo jema
- Awasihi wasisubiri kuona dalili za mvua ndio watengeneze barabara
- Asema huko ni kusababisha uharibifu kwakuwa mvua inazoa udongo
- KATIBU Mkuu, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Prof Riziki Shemdoe ametoa wito kwa wahusika wa utengenezaji barabara nchini hasa za kwenye mitaa, wakiwemo wasimamizi na wakandarasi wanaohusika kutengeneza barabara hizo kutosubiri kuona dalili za mvua ndipo waanze kutengeneza barabara.
- Amesema kufanya hivyo ni kuchangia uharibifu wa miundombinu hiyo, kwa sababu barabara zinapoanza kutengenezwa wakati mvua inanyesha au inakaribia kunyesha huishia kuharibika kutokana na ukweli kwamba katika hatua za awali tu za kuchongwa au kusawazishwa mvua huwa na nguvu ya kuondoa udongo wote unaokuwa umetifuliwa wakati wa kutengenezwa hivyo kuziweka barabara kwenye hali ya uharibifu zaidi.
- Prof Shemdoe amesema hivyo wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya ujenzi unaoendelea leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam. Mkutano huo ni wa siku mbili mfululizo; Disemba 15 na 16, mwaka huu.
- Amesisitiza uadilifu na kusema, “Tufanye kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia utaalamu”. Kwa maelezo ya Prof Mdoe Mkandarasi muadilifu hatasubiri kuona mvua ndio aende ‘site’ kutengeneza barabara, atafanya kazi hiyo kwa kuangalia muda na majira yanayofaa ili kuepuka kuchangua uharibifu.
- Mkutano huo umeandaliwa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ukiwa na mada mbili; ya kwanza inayozungumzia maendeleo ya sekta ya ujenzi Tanzania ikiangalia tulipotoka kisekta, tulipo na tunapoelekea pamoja na mada ya pili inayohusu maoni ya wadau yatakayosaidia kuanzishwa kwa kanuni za sheria ya NCC.
- Katika mada ya kwanza wadau wanajadili nini kifanyike ili kuivusha sekta kutoka katika hatua moja kwenda nyingine yenye maendeleo zaidi na katika mada ya pili, yanatafutwa maoni yatakayosaidia kupataa kanuni nzuri na zinazotekelezeka kwa ajili ya kuipa nguvu sheria ya NCC iliyopo.
- Mbali na Katibu Mkuu Shemdoe, baadhi ya wadau wamesema ili sekta hiyo ikue ni lazima pawepo dhamira ya dhati ya serikali ya kuikuza ikiwa ni pamoja na kukubali maoni mbalimbali ya wadau wa aina zote yenye mchango chanya katika sekta na kuyafanyia kazi kwa haraka iwezekanavyo.
- Miongoni mwa wadau hao ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi nchini, Arch Modest Maurus anayehusika na Shule ya Usanifu Majengo, Ukadiriaji na Usimamizi Majenzi (SACEM) katika chuo hicho aliyeiomba Serikali ibadili mfumo mzima wa elimu ya ufundi inayotolewa katika vyuo vya ufundi kwa sasa nchini ili iendane na wakati na mahitaji.
- Maurus ametoa mapendekezo hayo kwa niaba ya wanakikundi wote aliokuwa akijadili nao mambo mbalimbali yaliyoibua mawazo yao hayo katika mkutano huo, wakati wa kipindi cha majadiliano kwa vikundi.
- Amesema ipo haja kwa Serikali kubadili mfumo hasa kuanzia chuo (College) na Chuo Kikuu (University) ili kukidhi mahitaji yaliyopo na yanayojitokeza.
- Ametoa mfano wa eneo la uzalishaji mafundi mchundo ambao ndio watendaji wakuu katika miradi ya ujenzi na kusema kuwa mfumo wa sasa wa elimu umelenga kuwazalisha waelekezaji na kusahau watendaji, jambo linalotia shaka kwamba huenda tunapoelekea hatutakuwa na watendaji kazi hao muhimu (mafundi mchundo).
- “Vyuo vilivyokuwa vikizalisha mafundi mchundo sasa hivi karibu vyote vinazalisha wenye digrii. Maana yake karibu wote wanakuwa waelekezaji sasa ni nani atafanya kazi ‘site’?
Pia, Maurus pamoja na wenzake walipedekeza pamoja na mambo mengine, Tanzania iige mfuno wa wenzetu kwenye mabara mengine nje mfano Ulaya wa kuwatumia wataalamu wenye uzoefu walio mtaani bila kazi ili wawe kama watoa mada kwenye semina mbalimbali vyuoni, lengo likiwa kuhamisha maarifa yao na kushea mambo muhimu ya msingi ya kisekta kutokana na uzoefu wao.
Anasema wapo pia ambao si wataalamu kwa maana ya kupitia mafunzo ya chuo kikuu lakini wanauelewa na uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi ya ujenzi kwa vitendo, ambao Serikaliinaweza kuwatumia endapo itataka wafundishe wanavyuo masuala mbalimbali kwa vitendo hasa wanapofikia wakati wa kwenda ulingoni ‘field’.
Mwingine kati ya wengi waliochangia ni Mhandisi Edson Ngabo kutoka Wizara ya Nishati anayeelekeza mchango wake kwa taasisi na wizara zinazowakataa wanafunzi wanaotaka mafunzo kwa vitendo kupitia taasisi au wizara husika akiomba zielekezwe kuwakubali ili nao wajifunze kupitia taasisi au wizara hizo, waweze kukidhi kigezo cha uzoefu.
Mhandisi Ngabo amesema na kuuliza, “Kazi zikitangazwa zinaambatanishwa na kipengele kinachomtaka anayeiomba awe na uzoefu wa miaka mitatu au mitano, sasa huyu anatoa wapi huo uzoefu wakati katoka shule moja kwa moja na kila alipopeleka maombi ya kujiunga kama mwanafunzi anayefanyakazi kwa kujitolea ili angalau apate uzoefu anakataliwa?