​‘Rasimu ya mapendekezo gharama za ujenzi wa barabara tayari’

News Image May, 23 2023

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Mh. Prof Makame Mbarawa ameliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kwa Baraza hilo kukamilisha rasimu ya mapendekezo ya gharama za msingi za ujenzi wa barabara, kwa kila mkoa nchini.

Mh. Mbarawa ameeleza hayo bungeni wakati akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Katika hotuba yake, Waziri Mbarawa amelieleza Bunge kuwa Baraza la Taifa la Ujenzi, pamoja na mafanikio mengine, limekamilisha maandalizi ya kanuni zake na kutoa ushauri wa kitaalamu na kiufuindi kwa wadau wa sekta ya ujenzi nchini.

“Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako kuwa Baraza la Taifa la Ujenzi, kwa kushirikiana na Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), limekamilisha rasimu ya mapendekezo ya bei za msingi za ujenzi wa barabara kwa kila mkoa nchini, hivyo kuweza kuwa na mwongozo wa bei na gharama za ujenzi na ukarabati wa barabara nchini.

Kwa mujibu wake, NCC inatoa ushauri wa kiufundi kwa wadau wa sekta ya ujenzi nchini kwa lengo la kuongeza thamani ya mradi na kupunguza ongezeko la migogoro katika sekta ya ujenzi.

“Katika mwaka wa fedha 2022/23, Baraza la Taifa la Ujenzi limeratibu utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi na maridhianio, ambapo, migogoro mipya nane imepatiwa ufumbuzi, migogoro 17 inaendelea kutafutiwa ufumbuzi na kusajiliwa migogoro mipya 11.

Mbali na hayo, Mh Mbarawa ametaja Bungeni hapo kazi nyingine zilizofanywa na NCC kwa mwaka 2022/23 kuwa ni kuendelea na mapitio ya Sheria iliyoanzisha Baraza la Taifa la Ujenzi na kuandaa Kanuni zake; kuanza taratibu za kutunga Sheria ya Majengo (Building Act); kuandaa Taratibu za Majenzi (Building Codes) na Viwango Msawazo (Standard Specifications) kwa ajili ya majengo ya Serikali na samani; kuratibu utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi na maridhiano.

Baraza la Taifa la Ujenzi ndilo lenye jukumu la kushughulikia uratibu na uendelezaji wa Sekta ya Ujenzi nchini. Kazi zinazofanyika ni kutoa ushauri, miongozo ya kimkakati, uratibu wa shughuli za utafiti na mafunzo, ukusanyaji na uwekaji wa taarifa za ujenzi, tathmini ya utendaji kazi wa Sekta ya Ujenzi, uhamasishaji wa ubora wa kazi, ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa kiufundi na utatuzi wa migogoro ya ujenzi.