Bodi mpya ya NCC yazinduliwa

BODI mpya ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) imezinduliwa na tayari wajumbe wake wamekabidhiwa vitendea kazi, ili kuendelea kutekeleza majukumu waliyokwisha yaanza Julai Mosi, mwaka huu walipoteuliwa.
Bodi hiyo inayoongozwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Fatma Mohamed, ina wajumbe 12 kutoka fani mbalimbali wanaotajwa kuwa na ujuzi na weledi unaoweza kulisaidia Baraza la Taifa la Ujenzi kusonga mbele kimaendeleo na kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwemo kuishauri serikali mambo mbalimbali kuhusu maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.
Wajumbe hao 12 wanao mjumuisha Mwenyekiti ni pamoja na Mbunifu Majengo Oswald Modu kutoka OMG Consultants; Mkadiriaji Majenzi (QS) Justin Rwelengera kutoka Wither Limited, Sara Phoya ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Ardhi na Mkadiriaji Majenzi (QS) Optatus Kanyesi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Wengine ni Mhandisi, Prof John Bura ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa BQ Contractors Limited, Mhandisi Stephen Makigo kutoka Mayanga Contractors Limited, Kaimu Mkurugenzi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Awadh Salim, Dk Zacharia Katambara kutoka Chuo Kikuucha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Mhandisi Elisante Sumari kutoka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mhandisi Gwakisa Mwakyusa anayeiwakilisha sekta binafsi.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete ndiye aliyeizindua bodi hiyo jijini Dar es Salaam na kuitaka itumie weledi wa wajumbe wake kuhakikisha inaisimamia vizuri NCC iweze kutekeleza majukumu inayopaswa kuyafanya kwa faida ya taifa.