‘Ruhusuni majadiliano katika hali zote’
MWAKILISHI wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Subisi Mwasandenge, ametoa wito kwa viongozi wa chama hicho katika Tawi la Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) kuruhusu majadiliano wakati wote wanapokuwa katika hali zote, zikiwemo zisizovumilika.
Akizunguza katika ofisi za NCC jijini Dodoma, baada ya uzinduzi wa Tawi hilo la TUGHE ulioenda sambamba na uchaguzi wa viongozi, Mwasandenge amekiri kuwepo kwa vipindi vigumu amb apo menejimenti na wafanyakazi hushindwa kusikilizana, lakini akasema njia pekee inayoweza kutatua tatizo lolote kama lipo ni majadiliano na wala si vita.
Kwa mujibu wake, lengo la TUGHE ni kuhakikisha panakuwa na mazingira ya maeleweno kati ya menejimenti za taasisi za serikali au wizara na wafanyakazi wa taasisi au wizara husika, kutokana na usimamizi na utoaji wa haki kwa njia za kidemokrasia kwa pande zote mbili yaani wanamenejimenti pamoja na wafayakazi, na si mapigano.
“TUGHE inataka viongozi wote kuanzia ngazi ya juu hadi ya matawi kuzingatia thamani, kufuata na kutekeleza misingi ya demokrasia, ili kuendeleza amani na utulivu kati ya menejimenti na wafanyakazi...
Inategemewa kuwa viongozi wa Tawi la NCC waliochaguliwa wataitisha mikutano ya wafanyakazi baada ya kuwasiliana na mejimenti kuhusu haja hiyo, ili kusikia hoja zao, maoni yao na mahitaji yao. Pia, inategemewa kuwa watafikisha ujumbe wa wafanyakazi kwa menejimenti ili yanayotakiwa kujibiwa yajibiwe au yafanyiwe kazi,”amesema.
Neno kwa Menejimenti ya NCC
Mwasandenge aliyehusika kuandaa, kuratibu na kusimamia uchaguzi huo kwa niaba ya TUGHE Makao Makuu, ameishauri menejimenti iliyowakilishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Amosi Mazaba kuwapa wafanyakazi mrejesho kuhusu madai yao.
“Kwa kufanya hivyo, mtajenga maelewano ya hali ya juu na ushirikiano wenye tija kwa menejimenti na wafanyakazi huku mkiwa katika mazingira mazuri ya uelewano wenye tija”, amesema na kuongeza kuwa viongozi waliochaguliwa wana kazi ya ziada kuhakikisha watumishi ambao hadi sasa hawajajiunga na chama wanajiunga kwa faida yao wenyewe.
Katika uchaguzi huo uliohusisha upigaji kura, wamepatikana viogozi kwa nafasi mbalimbali kama zinavyo onekana katika mabano baada ya majina: Bi. Namsembaeli Mduma (Mwenyekiti), Bw. Tumaini Masige (Katibu), Bibi. Asina Mfinanga (Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake), Bi. Emma Mchome (Katibu wa Kamati ya Wanawake) na Bi. Ruth Mdenye (Mwakilishi wa Vijana).